Chanjo kutoka Afrika: Matumaini yapatikana
Tangu janga la Corona (UVIKO-19), Afrika imezindua mipango ya kutengeneza chanjo na dawa kwa ajili ya kuboresha huduma za afya. Ingawa mafanikio ya awali yanaonekana, lakini bado kunahitajika ufadhili wa muda mrefu.
Ripoti zinaonyesha kuwa, janga la COVID-19 limechochea harakati mpya barani Afrika za kujitegemea katika uzalishaji wa dawa na chanjo ili kupunguza utegemezi mkubwa wa uagizaji kutoka nje. Upungufu na usambazaji usio sawa wa chanjo wakati wa mlipuko huo uliweka wazi udhaifu wa mifumo ya afya barani humo na kuamsha dhamira ya kuwekeza zaidi katika sekta ya afya na teknolojia za tiba barani Afrika.
Mlipuko wa janga la COVID-19 mwaka 2020 ulidhihirisha kwa namna ya kutisha, utegemezi wa bara la Afrika kwa chanjo kutoka nje. Ingawa chanjo za COVID-19 zilichukuliwa kama hatua muhimu ya kudhibiti maambukizi, zilipatikana kwa upungufu mkubwa, zikisambazwa bila uusawa wala haki, na mataifa yenye kipato cha chini barani Afrika yalizipokea kwa kuchelewa sana.
Mtaalamu wa afya na mwanzilishi wa shirika la Medicines for Africa, Lenias Hwenda, anasema hali hiyo ilikuwa kengele ya tahadhari kwa bara zima. ''COVID-19 ilipelekea mabadiliko makubwa kwa viongozi wa Afrika.
Kabla ya janga hilo, hakukuwa na uelewa wa kutosha kuhusu jinsi gani bara hili lilivyokuwa hatarini kwa kutegemea uagizaji wa asilimia 99 ya chanjo na zaidi ya asilimia 90 ya dawa.''
Ripoti zinaonyeshha kuwa, mataifa ya Afrika sasa yameweka mikakati madhubuti ya kuongeza uzalishaji wa ndani wa dawa na chanjo ili kupunguza utegemezi wa muda mrefu. Nchini Senegal, Taasisi ya Pasteur imetengeneza chanjo ya homa ya manjano, huku Ghana, Nigeria, na Ivory Coast zikijenga viwanda vipya. Rwanda, kwa ushirikiano na kampuni ya Ujerumani ya BioNTech, inatarajia kuanza utengenezaji wa majaribio wa chanjo za mRNA mwaka huu, hatua inayotazamwa kama mfano wa mafanikio ya teknolojia ya hali ya juu.