Wanahabari wa Afrika waunda Muungano wa Kupinga Mauaji ya Kimbari ya Israel Gaza
Waandishi wa habari kutoka bara zima la Afrika wamezindua muungano uliopewa jina la 'African Journalists Against Genocide (AJAG)' wenye lengo la kupinga kile wanachoeleza kuwa ni mauaji ya kimbari ya Israel na uhalifu wa kivita dhidi ya watu wa Gaza, wakiwemo wanahabari wenzao.
Waandishi wa habari kutoka nchi zisizopungua 20 za Afrika wameungana chini ya bendera ya AJAG kuunga mkono juhudi za utetezi wa kimataifa zinazoishinikiza Israel kukomesha mauaji ya kimbari, ubaguzi wa rangi na kuikalia kwa mabavu Palestina.
Abdulrasheed Bala, mtafiti wa mawasiliano na mkuu wa Idara ya Uanahabari katika Chuo Kikuu cha Abubakar Tatari Ali huko Bauchi, Nigeria, amepongeza mpango huo na kusema, "Hii ni harakati muhimu sana ambayo inastahili kuungwa mkono. Tunazungumzia zaidi ya waandishi wa habari 272 na zaidi ya raia 62,000 waliouawa. Katika karne hii, dunia haijashuhudia uchokozi kama kile kinachotokea Gaza."
Amesema, "Tunalaani uvamizi wa Israel na tunaamini AJAG inaweza kuongeza ufahamu wa kimataifa, sio tu miongoni mwa waandishi wa habari na mashirika ya haki za kiraia, lakini duniani kote. Tunatoa wito kwa Umoja wa Mataifa kukomesha jinai huko Gaza."
Naye Anna Weeks, mwandishi wa habari wa Afrika Kusini na mwanachama wa AJAG ambaye aliitembelea Palestina mwanzoni mwa miaka ya 2000, amesema: "Ninalaani mauaji ya halaiki ya Wapalestina huko Gaza. Wakati huo pia, ilikuwa muhali kwa waandishi wa habari wa kimataifa kuingia (Gaza). Nilijaribu mara mbili sikufanikiwa. Israel lazima iruhusu waandishi wa habari kuingia na kukomesha sera ya njaa dhidi ya watu wa Gaza." Aliongeza, "Gaza kimsingi ni kambi ya mateso sasa. Watu wanakufa kwa njaa. Inatisha. Waandishi wa habari lazima wazungumze."
Kwa upande wake, Ernest Moloi, mwanachama wa AJAG kutoka Botswana, pia amelaani mauaji ya waandishi wa habari, wanawake, watoto, na wazee huko Gaza. Katika mahojiano na Iran Press, ameitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua dhidi ya kile alichokiita uchokozi unaoendelea wa Wazayuni.
Kutoka Harare, Zimbabwe, mwanachama mwingine wa AJAG, Munya Munaro amesema Israel lazima ibebe dhima. Amesisitiza kuwa, "Hili ni shambulio la wazi dhidi ya uandishi wa habari na ubinadamu. Ifahamike wazi, uandishi wa habari sio uhalifu."
Kwa mujibu wa Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari (CPJ), kati ya zaidi ya raia 62,000 walioripotiwa kuuawa shahidi na vikosi vya Israel huko Gaza, zaidi ya 274 walikuwa waandishi wa habari.