Wakimbizi wa Rwanda zaidi ya 500 warejea nchini kutoka Kongo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i129996-wakimbizi_wa_rwanda_zaidi_ya_500_warejea_nchini_kutoka_kongo
Wakimbizi wa Kinyarwanda zaidi ya 500 jana Jumatatu walirejea nyumbani wakitokea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2025-08-26T02:49:30+00:00 )
Aug 26, 2025 02:49 UTC
  • Wakimbizi wa Rwanda zaidi ya 500 warejea nchini kutoka Kongo

Wakimbizi wa Kinyarwanda zaidi ya 500 jana Jumatatu walirejea nyumbani wakitokea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Wakimbizi 533 wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto kwanza walisafirishwa hadi katika wilaya ya Rusizi magharibi mwa Rwanda kabla ya kuungana na jamii zao. Haya yameelezwa na Wizara Inayoshughulikia Masuala ya Dharura ya Rwanda. 

Hili ni kundi la kwanza la wakimbizi kusafirishwa hadi nyumbani chini ya makubaliano yaliyosainiwa mwezi jana kati ya Rwanda, Kongo na Kamisheni Kuu ya Wakimbizi ya UN kwa madhumuni ya kuheshimu haki za wakimbizi za kurejea kwa khiari katika nchi zao za asili. 

Wakimbizi hao 533 wa Kinyarwanda walikuwa wakiishi katika kambi za muda katika mji wa Goma, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambao unadhibitiwa na waasi wa M23. 

Katika andiko lake alilotuma katika mtandao wa X; Olivier Nduhungirehe Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda amesema: Licha ya makelele yanayopigwa na baadhi ya waharibifu wa nchi za Magharibi, ni vyema kutambua kwamba wakimbizi wa Rwanda, ambao wengi wao walikuwa wakishikiliwa mateka na kikosi cha mauaji ya kimbari cha FDLR mashariki mwa Kongo sasa wanaendelea kurejea nyumbani.”

Mwezi uliopita, Rwanda na Kongo  zilijitolea kuwezesha kurejea kwa usalama na kwa hiari wakimbizi hao kwa kuzingatia jitihada za hivi karibuni za kidiplomasia, hususan makubaliano ya amani yaliyofikiwa kati ya Kinshasa na Kigali, pamoja na tamko la kanuni zilizotiwa saini Julai 19 huko Doha kati ya serikali ya Kongo na waasi wa M23.