Botswana yatangaza dharura ya kiafya huku kukiwa na uhaba mkubwa wa dawa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i130016-botswana_yatangaza_dharura_ya_kiafya_huku_kukiwa_na_uhaba_mkubwa_wa_dawa
Botswana imetangaza dharura ya kiafya huku nchi hiyo ikikabiliwa na upungufu mkubwa wa dawa na vifaa tiba. Uhaba huo umesababisha hospitali na zahanati nchini humo kuhangaika kutibu magonjwa kuanzia shinikizo la damu, kisukari hadi saratani.
(last modified 2025-08-26T15:01:17+00:00 )
Aug 26, 2025 15:01 UTC
  • Botswana yatangaza dharura ya kiafya huku kukiwa na uhaba mkubwa wa dawa

Botswana imetangaza dharura ya kiafya huku nchi hiyo ikikabiliwa na upungufu mkubwa wa dawa na vifaa tiba. Uhaba huo umesababisha hospitali na zahanati nchini humo kuhangaika kutibu magonjwa kuanzia shinikizo la damu, kisukari hadi saratani.

Wizara ya Afya ya Botswana inasema kuwa uhaba wa dawa za matibabu na vifaa tiba umesabaishwa na  changamoto za kifedha. Rais wa nchi hiyo, Dumo Boko ameeleza kuwa kupanda kwa gharama za manunuzi na mifumo duni ya usambazaji vimesababisha hasara, upotevu na uharibifu.

Itakumbukwa kuwa, mapema mwezi huu wa Agosti, Wizara ya Afya ya Botswana ilitahadharisha kuhusu kupungua kwa akiba ya dawa na kuahirisha upasuaji wote ambao sio wa dharura.

Tangu wakati huo, Wizara ya Afya ya Botswana imepasisha pula milioni 250 ambazo ni sawa dola za Kimarekani milioni 17 kama fedha za dharura za kununulia vifaa tiba. 

Bajeti ya Botswana mwaka huu imekuwa chini ya mashinikizo makubwa kutokana na kudorora kwa muda mrefu kwa soko la almasi duniani. Botswana inaongoza kwa uzalishaji wa almasi kwa thamani.