Mahakama Kuu ya Kenya yaamuru kusitishwa ujenzi wa 'kanisa la Ruto, katika ikulu zote
Mahakama Kuu nchini Kenya imeamuru kusitishwa kwa muda ujenzi wa kanisa la kudumu au jengo lolote la kidini katika majengo ya Ikulu, jijini Nairobi. Agizo hilo la muda linazuia pia ujenzi kama huo katika Ikulu za Rais zilizoko maeneo mbalimbali nchini humo.
“Agizo la muda linatolewa kuizuia Serikali ya Kenya, maafisa wake, au yeyote kwa niaba yao, kujenga kanisa la kudumu au jengo lolote la kidini katika Ikulu ya Nairobi au katika Ikulu nyingine yoyote hadi Novemba 18, 2025,” alisema Jaji Chacha Mwita wakati akitoa amri hiyo.
Agizo hilo limetolewa kufuatia kesi iliyowasilishwa na mashirika manne ya kijamii ya Transparency International Kenya, Kenya Human Rights Commission, Inuka Kenya ni Sisi, na The Institute of Social Accountability, yaliyopinga hatua ya Rais William Ruto kuanzisha ujenzi wa kanisa ndani ya Ikulu ya Nairobi.
“Baada ya kuzingatia hoja za kesi na dharura ya jambo hili, ninaona kuwa ombi na kesi kuu zimeibua masuala muhimu ya kikatiba na kisheria yanayohusu uhusiano wa dini na serikali,” ameeleza hakimu huyo…/