Mkutano wa G20 nchini Afrika Kusini kuendelea hata kama Trump hatohudhuria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i130158-mkutano_wa_g20_nchini_afrika_kusini_kuendelea_hata_kama_trump_hatohudhuria
Afrika Kusini imesisitiza msimamo wake kwamba mkutano ujao wa nchi zilizostawi kiuchumi za G20, utakaofanyika Johannesburg mwezi Novemba, utaendelea kama ulivyopangwa; awepo au asiwepo Rais Donald Trump wa Marekani.
(last modified 2025-08-29T07:23:07+00:00 )
Aug 29, 2025 07:23 UTC
  • Mkutano wa G20 nchini Afrika Kusini kuendelea hata kama Trump hatohudhuria

Afrika Kusini imesisitiza msimamo wake kwamba mkutano ujao wa nchi zilizostawi kiuchumi za G20, utakaofanyika Johannesburg mwezi Novemba, utaendelea kama ulivyopangwa; awepo au asiwepo Rais Donald Trump wa Marekani.

Ronald Lamola, Waziri wa Mambo ya Nje, ameeleza kuwa Afrika Kusini imejizatiti kuhakikisha mkutano huo unafanikiwa, bila kujali kama Rais Trump atahudhuria binafsi au atamtuma mwakilishi.

Akizungumza na vyombo vya habari jijini Pretoria, Lamola amesema: “Tutaendelea na mkutano wa G20, awepo Rais Trump au la, au yeyote atakayemteua kuwakilisha Marekani.”

Trump awali alidokeza kuwa huenda asihudhurie mkutano huo, akitaja kile alichodai kuwa ni sera “mbaya sana” zinazotekelezwa na Afrika Kusini.

Lamola amesema hana uhakika kuhusu uamuzi wa mwisho wa Trump, akibainisha kuwa serikali ya Afrika Kusini bado inasubiri uthibitisho rasmi.

Ameongeza: “Hali hii si ya kutabirika. Tutasubiri kauli ya mwisho kutoka Marekani pale watakapofanya uamuzi. Bila kujali uamuzi wao, mkutano wa G20 utaendelea. Tutashirikiana na viongozi wote watakaokuwepo kuamua mwelekeo wa majadiliano.”

Kuhusu ushuru wa asilimia 30 uliowekwa na Marekani dhidi ya bidhaa za Afrika Kusini, Lamola amesema kuwa serikali yake inaendelea na juhudi za kidiplomasia kwa ajili ya kupunguza ushuru huo. Ameongeza kuwa Afrika Kusini inapanua masoko yake kuelekea Mashariki na nchi nyingine zinazodumisha uhusiano wa kibiashara, bila kutegemea Marekani pekee.

Kuhusiana na uamuzi wa awali wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kuhusu Israel, Lamola amesisitiza umuhimu wa kuheshimiwa sheria za kimataifa.

Afrika Kusini imefungua kesi dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), kuhusu mashambulizi ya “mauaji ya kimbari” dhidi ya Gaza, ambayo hadi sasa yamesababisha vifo vya zaidi ya Wapalestina 63,000.

Pia, Waziri Lamola amezungumzia mpango wa Marekani wa kuharakisha mchakato wa uhamiaji kwa Waafrika Kusini wenye asili ya Kizungu (Afrikaners), akikanusha madai kuwa ni wakimbizi.

Amesema: “Hatuafiki kuwa huu ni mpango wa wakimbizi kwa sababu hakuna mauaji ya kimbari Afrika Kusini.”