Mapigano ya ndani Sudan Kusini yaibua hofu kuhusu makubaliano tete ya amani
Mapigano ya siku mbili kati ya vikosi vya jeshi la serikali na wapiganaji waasi nchini Sudan Kusini yamezua hofu kuhusu makubaliano tete ya amani ya nchi hiyo.
Ni baada ya Sudan People’s Liberation Army in Opposition (SPLA-IO) kuvituhumu vikosi vya serikali ya Sudan Kusini kwamba vimeanzisha mashambulizi dhidi ya wapiganaji wake Magharibi mwa majimbo ya Equatoria na Upper Nile.
Msemaji wa kundi hilo amesema, mpiganaji mmoja wa waasi na wanajeshi wawili wameuawa katika mapigano hayo na wengine kadhaa wamejeruhiwa.
SPLA-IO imesema mashambulizi hayo ni ukiukaji wa wazi wa makubaliano ya amani ya 2018 yenye lengo la kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vya umwagaji damu kati ya serikali ya Rais Salva Kiir na vikosi vinavyomtii makamu wake wa zamani, Riek Machar.
Mvutano umekuwa ukiongezeka nchini humo tangu mwezi Machi, wakati jeshi lilipoanzisha operesheni kadhaa kwenye maeneo ya raia. Ripoti za kuwepo wanajeshi wa Uganda wanaolisaidia jeshi la serikali ya Sudan Kusini pia zimezidisha hofu ya kutokea tena vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Mwezi Machi mwaka huu, Riek Machar, ambaye anahudumu kama Makamu wa Rais katika serikali ya kugawana madaraka, alikamatwa kwa kuzungumza dhidi ya ripoti za wanajeshi wa Uganda wanaolisaidia jeshi. Umoja wa Mataifa ulisema kukamatwa kwake kumeiweka nchi ya Sudan Kusini kwenye ukingo wa migogoro mikubwa zaidi.