Misri: Hatutakuwa lango la kupitishia Wapalestina wanaohamishwa kwa nguvu katika ardhi yao
Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imelaani matamshi ya waziri mkuu wa utawala wa kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu na kusisitiza kuwa Misri haitakuwa lango la kupitishia wananchi wa Palestina wanaohamishwa kwa nguvu katika ardhi yao.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imeeleza hayo kupitia taarifa na kutangaza kuwa inapinga vikali jaribio lolote na linalofanywa kwa anuani yoyote, la kuwahamisha Wapalestina katika ardhi yao.
Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, Misri kamwe haitakuwa mshirika wa kufuta piganio tukufu la Wapalestina na haitakuwa lango la kupitishia wananchi hao, na kwamba huo ni mstari mwekundu usioweza kubadilika.
Kadhalika, taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imetoa wito wa kukabiliana na hali ya machafuko iliyoanzishwa na utawala wa kizayuni wa Israel katika eneo na kutahadharisha juu ya madhara yake kwa usalama na uthabiti wa eneo hili.
Wakati huohuo, ofisi ya waziri mkuu wa utawala ghasibu wa Israel Benjamin Netanyahu imetoa majibu kwa taarifa hiyo ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri kuhusu kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina wa Ghaza kupitia kivuko cha Rafah.
Ofisi hiyo ya Netanyahu imedai kwamba waziri mkuu huyo wa utawala wa kizayuni ametoa matamshi kuhusu kuhama Wapalestina wa Ghaza kwa kutetea haki za binadamu za kila mtu kuchagua kwa uhuru makazi yake.
Netanyahu alidai katika mahojiano na chombo cha habari cha Telegram kwamba nusu ya wakazi wa Ukanda wa Ghaza wanataka kulihama eneo hilo na kwamba angewafungulia kivuko cha Rafah lakini anaamini akifanya hivyo, Misri itakifunga papo hapo kivuko hicho.
Matamshi ya Netanyahu ya kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina wa Ukanda wa Ghaza ikiwemo kupitia kivuko cha Rafah ambacho ni mpaka wa pamoja wa ukanda huo na Misri yamelaaniwa vikali na serikali za Misri, Qatar na Saudi Arabia.../