Araghchi katika mazungumzo na Mufti Mkuu wa Tunisia: Kukomeshwa mauaji ya halaiki huko Gaza kunahitajia ushirikiano wa Umma wa Kiislamu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i130684-araghchi_katika_mazungumzo_na_mufti_mkuu_wa_tunisia_kukomeshwa_mauaji_ya_halaiki_huko_gaza_kunahitajia_ushirikiano_wa_umma_wa_kiislamu
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika kikao na Mufti Mkuu wa Tunisia kwamba: "Kukomeshwa mauaji ya halaiki ya utawala wa Kizayuni huko Gaza na kuzuia kupanuka kwa wigo wa uchokozi wa utawala huo kunahitajia ushirikiano mkubwa wa Umma wa Kiislamu."
(last modified 2025-09-11T12:50:08+00:00 )
Sep 11, 2025 12:50 UTC
  • Araghchi katika mazungumzo na Mufti Mkuu wa Tunisia: Kukomeshwa mauaji ya halaiki huko Gaza kunahitajia ushirikiano wa Umma wa Kiislamu

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika kikao na Mufti Mkuu wa Tunisia kwamba: "Kukomeshwa mauaji ya halaiki ya utawala wa Kizayuni huko Gaza na kuzuia kupanuka kwa wigo wa uchokozi wa utawala huo kunahitajia ushirikiano mkubwa wa Umma wa Kiislamu."

Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ambaye amefanya safari nchini humo kwa ajili ya kushauriana na viongozi waandamizi wa serikali ya Tunisia, amekutana na kuzungumza pia na Sheikh Hisham Mahmoud Mufti Mkuu wa Tunisia Jumatano jioni katika maadhimisho ya maulidi ya Mtume Mtukufu (saw). Huku akiwapongeza wananchi na serikali ya Tunisia kwa mnasaba huo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesisitiza juu ya ulazima wa kuwepo umoja wa Waislamu kote ulimwenguni chini ya miongozo na mafundisho ya Mtume Mtukufu wa Uislamu. Ameashiria kuendelea jinai za utawala wa Kizayuni huko Gaza na kupanuka kwa wigo wa uchokozi wake katika eneo zima la Asia Magharibi. Amesisitiza juu ya udharura wa kusimamishwa mara moja mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Gaza na kusema suala hilo linahitajia ushirikiano na uratibu wa dhati wa Umma wa Kiislamu.

Mufti Mkuu wa Tunisia pia ameelezea kufurahishwa kwake na uwepo wa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran katika Msikiti Mkuu wa Ez-Zaituna na kufafanua historia ya msikiti huo na umuhimu wake katika kueneza Uislamu nchini Tunisia, Afrika Kaskazini na ulimwengu mzima wa Kiislamu.

Kisha Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ametembelea na kukagua kumbi tofauti za msikiti huo. Msikiti Mkuu wa az-Zaitouna ni miongoni mwa misikiti mikongwe zaidi nchini Tunisia yenye hadhi na nafasi ya kihistoria, ambao ulijengwa mwaka 79 Hijria na katika historia yake ndefu, umekuwa na nafasi muhimu sana katika kueneza mafundisho na maarifa ya Kiislamu.