Wanigeria waandamana kulaani shambulio la Israel dhidi ya msafara wa Sumud
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i131570-wanigeria_waandamana_kulaani_shambulio_la_israel_dhidi_ya_msafara_wa_sumud
Waislamu kote nchini Nigeria waliingia barabarani baada ya Swala ya Ijumaa hapo jana kulaani shambulio la Israel dhidi ya msafara wa kimataifa wa Sumud, wenye makumi ya meli zinazoelekea katika Ukanda wa Gaza.
(last modified 2025-10-04T06:04:45+00:00 )
Oct 04, 2025 06:04 UTC
  • Wanigeria waandamana kulaani shambulio la Israel dhidi ya msafara wa Sumud

Waislamu kote nchini Nigeria waliingia barabarani baada ya Swala ya Ijumaa hapo jana kulaani shambulio la Israel dhidi ya msafara wa kimataifa wa Sumud, wenye makumi ya meli zinazoelekea katika Ukanda wa Gaza.

Katika Jimbo la Bauchi, kaskazini mashariki mwa Nigeria, idadi kubwa ya wanaume, wanawake na watoto walishiriki na maandamano hayo, wakiwa wamebeba bendera za Palestina na kupiga nara za kupinga mauaji ya halaiki huko Gaza.

Waandamanaji wamelaani vikali kitendo cha utawala ghasibu wa Israel cha kuuvamia kijeshi msafara wa kimataifa wa meli unaojulikana kama Sumud uliokuwa ukielekea Ukanda wa Gaza kwa ajili ya kufikisha misaada ya kibinadamu na kuvunja mzingiro wa Tel Aviv dhidi ya ukanda huo.

Boti nyingi za msafara wa kimaataifa wa meli zipatazo 50 unaojulikana kama (Sumud) zilivamiwa hivi karibuni na jeshi la wanamaji la Israel zilipokuwa zikikaribia katika ukanda huo wa pwani.

Idadi isiyojulikana ya wanaharakati wa msafara huo wa kimataifa walitiwa mbaroni na mawasiliano ya meli hizo na ulimwengu wa nje yalikatizwa na jeshi la lsrael.

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa siku ya Alkhamisi alitaka kuachiliwa mara moja kwa Waafrika Kusini na raia wengine wa kigeni wanaozuiliwa na jeshi la Israel, baada ya wanajeshi wa majini wa utawala huo haramu kushambulia msafara wa kibinadamu uliokuwa unaelekea Gaza.

Ramaphosa amelaani shambulio hilo katika maji ya kimataifa, akisema linaonyesha kuendelea kwa Israel kupuuza sheria za kimataifa sanjari na kushtadi mgogoro wa kibinadamu katika eneo hilo la Palestina linalozingirwa.