Vikosi vya usalama vya Kongo vyashutumiwa kwa unyanyasaji
Tangu mapema mwezi huu wa Oktoba, kikosi cha ulinzi wa rais wa Kongo Brazzaville kimeanzisha operesheni dhidi ya magenge ya wahalifu ya vijana wanaoshambulia watu kwa mapanga wanaojulikana kwa jina maarufu la 'bebe noir' au watoto weusi.
Makundi hayo yamekuwa yakieneza ugaidi katika miji mikubwa ya nchi hiyo kwa miaka kadhaa, yakishambulia na kuiba kwenye maduka ya biashara na majumbani.
''Ni mpango mzuri kwa sababu wananchi wa Kongo daima wanaogopa kutoka nje. Natumai operesheni hii itadumu," amesema mkazi mmoja wa Pointe-Noire kusini mwa Kongo Brazzaville.
“Hivi sasa sisi wenye maduka tunalazimika kufunga mapema kuliko tulivyopanga, vinginevyo wanaiba fedha zetu au kutuua kwa mapanga,” amesema mfanyabiashara mmoja wa rejaraja.
Ingawa wengi wanaiunga mkono operesheni hiyo ya kudhibiti genge hilo lakini wengine wanalalamikia njia zinazotumika baada ya kuenea picha za kutisha za mauaji ya watu kwenye mitandao ya kijamii. Wanaharakati wa haki za binadamu wamelalamikia kile wanachokiita mtafaruku hatari unaokanyaga katiba ya Kongo Brazzaville.
'Bebe noir' wengi wao ni vijana wenye umri wa kati ya miaka 13 na 30. Mwendesha mashtaka huko Brazaville, mji mkuu wa Kongo ameuita uhalifu wao kuwa ni 'ugaidi'.
Ukosefu wa ajira uliokithiri umetajwa kuwa ndiyo sababu ya kuongezeka vitendo vya uhalifu na vya kikatili huko Kongo Brazzaville, nchi ambayo ni mzalishaji mkubwa wa mafuta. Ingawa Kongo ilipiga marufuku hukumu ya kifo mwaka 2015, lakini mauaji ya kiholela yanazidisha hali ya hofu na unyanyasaji. Serikali imeamua kujenga kituo cha kuunganisha upya vijana na hivi sasa kinakaribia kufunguliwa. Kituo hicho kimejengwa katika eneo la Bouenza lililoko umbali wa kilomita 200 kutoka Brazzaville.