Misri na vita vya Gaza; Kujaribu kufuata mkakati wa uwastani
Kuanza vita vya Gaza baada ya operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa mnamo Oktoba 7, 2023 ulikuwa mwanzo wa mabadiliko katika sera za ndani na za kigeni za Misri.
Kufuatia operesheni hiyo, Misri ilikabiliwa ghafla na hali ambayo iliiweka kwenye mashinikizo makubwa ya ndani na nje na kutishia kuathiri vibaya nafasi yake ya kikanda na kihistoria. Hali ambayo si tu ilihitaji majibu ya haraka ya kiusalama na kidiplomasia, bali pia ililazimu kubuniwa mkakati wa muda mrefu kwa ajili ya kudumisha nafasi ya jadi ya Misri katika kadhia nzima ya Palestina.
Kuhusu vita vya Gaza, Misri imekabiliwa na changamoto nyingi kama vile mashinikizo ya kimataifa, masuala ya usalama wa ndani na kujitolea kwa ajili ya kadhia ya Palestina. Misimamo na hatua za Misri kuhusu vita vya Gaza zinaweza kuorodheshwa katika mihimili kadhaa muhimu kama ifuatavyo:
Kudhibiti maoni ya umma na kusimamia migogoro ya kisiasa
Maoni ya umma ya Misri yanafungamana kihistoria na suala la Palestina, hivyo kuongezeka mgogoro wowote huko Gaza unaweza kuchochea hasira ya wananchi na maandamano ya nchi nzima. Kufuatia matukio ya Oktoba 7, wimbi la mshikamano na Wapalestina liliibuka miongoni mwa watu wa Misri, suala ambalo lingeweza kuyumbisha kirahisi hali ya kisiasa ya ndani.
Serikali ya Misri ilidhibiti kwa uangalifu mkubwa mikusanyiko ya raia na kuzuia kuenea kwake kwa kutumia vyombo vya habari na vikwazo vya usalama. Udhibiti huo ulifanyika kwa malengo mawili makuu: Kuzuia kuibuka mgogoro wa kisiasa na kudumisha utulivu wa umma bila kuchukua msimamo hasimu dhidi ya Palestina mbele ya maoni ya umma.
Uwastani katika kushughulikia mahitaji kinzani ya kigeni
Katika medani ya kimataifa, Misri ilikuwa katika hali ngumu sana. Wahusika mbalimbali wa kimataifa na kieneo, hususan serikali za Magharibi na baadhi ya nchi za Kiarabu, zilichukua misimamo dhidi ya Hamas na muqawama na kuishinikiza Misri itekeleze siasa zake kwa maslahi ya usalama wa Israel. Katika upande wa pili, nchi huru na makundi ya Misri yaliitaka serikali kuchukua msimamo madhubuti na wa wazi zaidi katika kuitetea Palestina. Kuhusiana na suala hilo, jibu la Cairo llikuwa mchanganyiko mzuri: Kulaani hadharani mashambulio ya Israel, kuchukulia kuhamishwa kwa nguvu watu wa Gaza kama mstari mwekundu na usioweza kujadiliwa kwa Misri, kuishinikiza Israel ikubali usitishaji mapigano na kuchukua hatua za kivitendo kwa ajili ya kutumwa misaada ya kibinadamu huko Gaza. Sera hii iliweza kudhibiti kwa kiasi fulani matakwa ya pande zote mbili na hivyo kuzuia makabiliano ya moja kwa moja na moja ya pande zilizokuwa zikitoa matakwa kinzani.

Jukumu la pande mbili la Misri; Ulindaji mpaka na upatanishi usio na matunda
Kama jirani wa Ukanda wa Gaza, Misri imekuwa na majukumu mawili makuu. Kwa upande mmoja, kudhibiti kivuko cha Rafah, njia pekee ya Gaza kuelekea ulimwengu wa nje, kumeifanya nchi hii kuwa "mlinda lango" wa masuala ya kibinadamu wa eneo hilo. Kufungua au kufunga kivuko hiki daima limekuwa suala muhimu katika ufikishaji misaada na pia harakati za watu. Katika upande pili, Misri ina historia ndefu ya upatanishi kati ya Israel na makundi ya Wapalestina na imekuwa mwenyeji wa mazungumzo ya kusitisha mapigano katika nyakati tofauti, vikiwemo vita vya Gaza vya 2014 na mazungumzo ya hivi karibuni. Pamoja na hayo lakini nafasi hii haijafanikiwa siku zote. Sasa, Misri na Qatar zinafanya juhudi za kufanikisha usitishaji vita huko Gaza.
Usalama wa taifa; Kufurushwa Wapalestina mstari mwekundu kwa Cairo
Wasiwasi muhimu zaidi wa Misri katika mazingira ya vita vya Gaza ni usalama wake wa taifa. Cairo inapinga vikali mpango wowote wa kuhamisha Wapalestina kwa nguvu kutoka Gaza hadi Jangwa la Sinai, na kuuchukulia kuwa tishio la moja kwa moja kwa mamlaka yake ya kujitawala na utulivu wa ndani. Viongozi wa Misri wanachukulia hali hii kuwa "tishio la moja kwa moja kwa usalama wa taifa" kwa sababu inaweka mzigo mzito wa kibinadamu na kiusalama kwenye mabega ya nchi hiyo. Hata kuna tetesi kwamba Marekani inaweza kushughulikia utatuzi wa mgogoro wa Bwawa la Ennahda kati ya Ethiopia na Misri iwapo Cairo itakubali Wapalestina kuhamishiwa katika Jangwa la Sinai, suala ambalo Misri inalikanusha vikali.
Wasiwasi huu umepelekea jeshi la Misri kuimarisha kwa kiasi kikubwa uwepo wake kwenye mpaka na Gaza ili kuzuia kuhatarishwa usalama na wakati huo huo kutuma ujumbe wa wazi wa kisiasa kwa Israel kwamba haitakubali kubebeshwa mzigo na gharama yoyote kuhusu suala hilo.
Mashinikizo ya kiuchumi na zana za ushawishi
Utawala wa Kizayuni umetumia njia za kiuchumi kutoa mashinikizo dhidi ya Misri. Mfano wa wazi wa hilo ni kusitishwa kwa mkataba wa gesi wa dola bilioni 35 na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, ambao ulikuwa umetiwa saini mwezi mmoja kabla. Madhumuni ya hatua hii ni kuilazimisha Misri ilegeze msimamo kuhusu kupeleka vikosi vyake huko Sinai, kuongeza mashinikizo dhidi ya Hamas na kuifanya ilainishe msimamo kuhusu kuhamishwa kwa nguvu Wapalestina kutoka Gaza.
Hatua hii inaonyesha wazi jaribio la Israel la kutumia masuala ya kiuchumi kama chombo cha kuendeleza malengo yake ya kisiasa na kiusalama katika eneo.
Muhtasari
Kwa ujumla, msimamo wa Misri kuhusu vita vya Gaza unaweza kuchukuliwa kama mchanganyiko wa mshikamano na watu wa Palestina, kufanya mahesabu magumu ya usalama wa taifa na kujaribu kuwa mhusika muhimu mwenye busara katika jukwaa la kimataifa. Sera hii imekuwa ikifuatwa kwa kutumia zana za kidiplomasia, kiusalama na kiuchumi ili kuiwezesha Cairo kudumisha nafasi yake muhimu katika matukio ya Palestina na Gaza. Hivyo, ni wazi kuwa kivuko cha Rafah, upatanishi wa usitishaji vita na kukabiliana vilivyo na uhamiaji wa lazima wa Wapalestina ni mihimili mitatu mikuu ya sera za Misri kuhusu vita vya Gaza, ambavyo bila shaka vitaathiri mustakbali wa nchi hiyo na eneo zima kwa ujumla.