Putin: Suluhisho la kadhia ya nyuklia ya Iran ni mazungumzo
Katika mazungumzo ya simu na Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, Rais Vladimir Putin wa Russia amesisitizia ulazima wa kutatuliwa suala la nyuklia la Iran kwa njia ya mazungumzo na ndani ya fremu ya sheria za kimataifa.
Shirika la Habari la Fars limenukuu taarifa ya Ikulu ya Rais wa Russia, Kremlin ikitangaza usiku wa kukamkia leo kwamba Rais Vladimir Putin na waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu wamefanya mazungumzo ya simu na kujadiliana matukio ya hivi karibuni katika eneo la Asia Magharibi, hasa hali ya Ukanda wa Ghaza ndani ya fremu ya mpango wa hivi karibuni wa kusimamisha vita uliopendekezwa na rais wa Marekani.
Taarifa ya Kremlin imesema: "Putin kwa mara nyingine ametilia mkazo msimamo thabiti wa Russia wa kuunga mkono suluhisho la kina la suala la Palestina kwa kuzingatia mfumo wa kisheria unaotambuliwa kimataifa." Taarifa hiyo imesema kuwa, pande hizo mbili zimebadilishana mawazo pia kuhusu masuala mengine ya kikanda. Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Kremlin, Rais wa Russia amesisitizia haja ya kutafutwa suluhisho la amani la mpango wa nyuklia wa Iran na kuimarisha utulivu nchini Syria.
Mazungumzo hayo ya simu yamefanyika usiku wa kuamkia mwaka wa pili wa vita vya kinyama vya Israel katika Ukanda wa Ghaza, vita ambavyo vimeshapelekea zaidi ya Wapalestina 67,000 kuuawa shahidi wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto wadogo.
Hayo yamekuja huku wajumbe wa utawala wa Kizayuni na Hamas wakianza mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja jana Jumatatu katika mji wa Sharm el-Sheikh nchini Misri kuhusu mpango wenye vipengele 20 wa Donald Trump, uliotangazwa tarehe 29 Septemba.