Rais wa Madagascar kufanya mazungumzo ya kitaifa leo
Rais Andry Rajoelina wa Madagascar amesema anapanga kufanya "mazungumzo ya kitaifa" na makundi mbalimbali leo Jumatano baada ya vijana waandamanaji kutoa makataa ya saa 48 ili akubali matakwa yao la sivyo akabiliwe na maandamano ya kitaifa.
Mazungumzo yaliyopangwa leo alasiri yatahudhuriwa na viongozi wa kidini, wanafunzi, wawakilishi wa vijana, na makundi mengine.
Tangazo hilo la Rais Rajoelina limekuja siku moja baada ya kumteua Jenerali Ruphin Fortunat Zafisambo kuwa Waziri Mkuu mpya wa nchi hiyo wiki moja baada ya kulivunja baraza la mawaziri kufuatia maandamano ya wananchi ya siku kadhaa.
Maandamano nchini Madagascar ambayo yalikuwa yameingia katika wiki ya tatu yalisababishwa na kutoridhishwa wananchi na kukatika pakubwa huduma za umeme na maji nchini humo.
Akihutubia siku ya Jumamosi, Rais wa Madagascar alieleza kuwa yupo tayari kusikiliza matakwa ya wananchi. Hata hivyo alipuuzilia mbali wito wa kujiuzulu na kuwatuhumu mahasimu wake kuwa wana lengo la kuipindua serikali yake.
Akizungumza siku ya Jumatatu na wawakilishi wa jumuiya za kiraia, Rais wa Madagascar alisema kuwa hana nia ya kugombea kiti cha urais kwa muhula wa tatu.
Maandamano hayo yanayoongozwa na Gen-Z yamekuwa yakiendelea Madagascar kwa wiki kadhaa sasa na yalichochewa na ghadhabu za wananchi wanaolalamikia uhaba wa maji na umeme.
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa mgogoro wa Madagascar umesababisha vifo vya watu wasiopungua 22 na kujeruhiwa zaidi ya 100 katika kile kinachotajwa kama changamoto kubwa zaidi kuukabili utawala wa Rajoelina baada ya miaka kadhaa.