Umoja wa Mataifa wataka njia salama kwa raia waliokwama el-Fasher, Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i132490-umoja_wa_mataifa_wataka_njia_salama_kwa_raia_waliokwama_el_fasher_sudan
Umoja wa Mataifa umezitolea mwito pande zinazopigana nchini Sudan kuhakikisha raia waliokwama katika mji wa el-Fasher wanapatiwa njia salama ya kuondoka, baada ya wapiganaji wa kundi la Rapid Support Forces (RSF) kutangaza kuwa wametwaa udhibiti wa kambi kuu ya jeshi katika mji huo.
(last modified 2025-10-28T03:14:03+00:00 )
Oct 28, 2025 03:14 UTC
  • Umoja wa Mataifa wataka njia salama kwa raia waliokwama el-Fasher, Sudan

Umoja wa Mataifa umezitolea mwito pande zinazopigana nchini Sudan kuhakikisha raia waliokwama katika mji wa el-Fasher wanapatiwa njia salama ya kuondoka, baada ya wapiganaji wa kundi la Rapid Support Forces (RSF) kutangaza kuwa wametwaa udhibiti wa kambi kuu ya jeshi katika mji huo.

Jeshi la Sudan halijathibitisha kupoteza kambi hiyo, jambo ambalo, likithibitishwa, litakuwa ushindi mkubwa kwa wanamgambo wa RSF katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea nchini humo.

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, amesema mapigano hayo mapya ni “ongezeko baya mno la machafuko,” na kuongeza kuwa mateso wanayopitia raia  “hayavumiliki,”.

El-Fasher, ambayo ni ngome ya mwisho ya jeshi la Sudan katika eneo pana la magharibi mwa Darfur, imekuwa chini ya mzingiro wa RSF na washirika wake kwa zaidi ya miezi 18.

Mapigano makali yalizuka tangu Jumamosi, baada ya wapiganaji wa RSF kuteka makazi ya gavana wa jimbo la Kaskazini mwa Darfur.

Wanamgambo wa RSF wanadai kudhibiti mji mzima, lakini washirika wa kijeshi wa serikali katika eneo hilo wanasema mapigano bado yanaendelea katika baadhi ya mitaa.

Kundi hilo limekosolewa kwa kushambulia raia kwa mabomu ya angani na kuwazuilia takribani watu 250,000, baada ya kuuzungushia mji huo ukuta wa udongo, hali iliyowaacha wengi katika njaa kali na kukosa msaada wa kibinadamu.

Mji wa el-Fasher sasa unatajwa kuwa moja ya maeneo yenye mapigano makubwa zaidi katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan, ambapo Umoja wa Mataifa umeueleza kama “kitovu cha mateso.”