Hali bado si shwari Tanzania, matokeo yakiendelea kutangazwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i132640-hali_bado_si_shwari_tanzania_matokeo_yakiendelea_kutangazwa
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania inaendelea kutangaza matokeo ya awali ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika 29 Oktoba, 2025.
(last modified 2025-10-31T16:45:06+00:00 )
Oct 31, 2025 12:12 UTC
  • Hali bado si shwari Tanzania baada ya uchaguzi wa Oktoba 29
    Hali bado si shwari Tanzania baada ya uchaguzi wa Oktoba 29

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania inaendelea kutangaza matokeo ya awali ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika 29 Oktoba, 2025.

Matokeo hayo yamepokelewa kutoka maeneo bunge mbalimbali.

Kwa mujibu wa matokeo ya awali yanayoendelea kutangazwa na Tume ya Uchaguzi, mgombea wa Chama tawala nchini humo CCM Mama Samia Suluhu Hassan yuko kifua mbele.

INEC ilikuwa imesema kuwa itamtangaza mshindi wa urais ndani ya saa 72 baada ya uchaguzi kufanyika 29/10/2025.

Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, maandamano na vurugu za hapa na pale zimeendelea kushuhudiwa katika baadhi ya maeneo ya Tanzania.

Chama kikuu cha upinzani Tanzania CHADEMA, kimedai kuwa, takriban watu 700 wameuwawa ndani ya siku tatu za ghasia za baada ya uchaguzi. Mtandao umeendelea kuminywa nchini Tanzania kwa siku ya tatu na kufanya mawasiliano kuwa magumu. Hayo yameelezwa na msemaji wa Chadema John Kitoka.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema kuwa, limepokea taarifa kuwa karibu watu 100 wamefariki dunia.

Hapo jana, ulionekana kurejea kwa muda kidogo tu kama takriban saa moja hivi kabla ya kuanza tena kuminywa.

Mkuu wa jeshi nchini Tanzania amelaani vitendo vya vurugu katika baadhi ya mikoa na kuvitaja kuwa kinyume cha sheria.

Mama Samia Suluhu Hassan, mgombea wa chama tawala CCM akipiga kura (29 Oktoba, 2025)

Katika hotuba yake iliyorushwa na televisheni ya taifa, Jenerali Jacob John Mkunda alisema ni 'lazima utawala wa sheria uzingatiwe' na kuonya kuwa wahusika watachukuliwa hatua.

Mapema leo Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally aliwataka  Waislamu kuswali swala ya adhuhuri nyumbani badala ya kwenda msikitini.

Huku hayo yakiarifiwa vyaombo vya habari vya ndani ya Tanzania vimebakia kimya kuhusu zoezi la uchaguzi, huku Rais Samia Suluhu Hassan akiwa bado hajaonekana hadharani wala kusema chochote tangu alipopiga kura siku ya uchaguzi. Kwa Upande wa Zanzibar, Tume ya Uchaguzi ZEC jana ilimtangaza Hussein mwinyi kuwa mshindi wa kiti cha urais, tangazo ambalo limepingwa na wafuasi wa chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo ambao wanadai zoezi hilo halikuwa uchaguzi bali uchafuzi.

Wafanyabiashara, wasanii na rai wa kawaida wameripoti kupata hasara ya biashara, nyumba na milki zao baada ya vijana wanaopinga uchaguzi kuharibu mali zao.

Wadadisi wa mambo wanayataja matukio ya mara hii nchini Tanzania kwamba, hayajawahi kushuhudiwa katika chaguzi zote zilizofanyika nchini humo.