IEBC yawataka wanasiasa wa Kenya wasichochee machafuko na uvunjivu wa amani
-
Wanasiasa wanakiwa kuacha uchochezi wa machafuko
Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya (IEBC), imewataka wanasiasa kuelekeza nguvu zao katika kuhimiza amani na utulivu, badala ya kutoa matamshi yanayoweza kuchochea taharuki miongoni mwa wananchi.
Kamishna wa IEBC, Dkt Alutalala Mukhwana, amesema baadhi ya matamshi yanayotolewa na viongozi wa kisiasa, hasa yanayoonesha shaka kuhusu uwezo wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka kusimamia uchaguzi huru na wa haki, yanaweza kuathiri mtazamo wa umma na kuzua hali ya kutoaminiana bila sababu.
Alikuwa akizungumza katika kikao na wanahabari mjini Hola, Kaunti ya Tana River katika siku ya mwisho ya kampeni za chaguzi ndogo zitakazofanyika maeneo tofauti nchini Kenya Novemba 27, 2025.
“Kila maoni ya kutilia shaka taasisi ya uchaguzi yanaathiri wananchi moja kwa moja. Tunawaomba wanasiasa kupunguza joto la kisiasa na kuanza kuhubiri amani,” amesema Alutalala Mukhwana.
Matamshi hayo yametolewa baada ya chama cha DCP kinachoongozwa na aliyekuwa naibu rais wa Kenya, Bw Rigathi Gachagua, kiibua madai kuhusu ukosefu wa uaminifu katika uchaguzi mdogo wa Magarini kwenye kaunti ya Kilifi.
Uchaguzi huo ulio na wagombeaji 10 umevutia ushindani mkali kati ya Harrison Kombe wa chama cha ODM, na Stanley Kenga wa DCP.
Dkt Alutalala Mukhwana ameahidi kuwa IEBC itahakikisha uwazi, uadilifu na kuzingatia sheria katika kila hatua ya mchakato wa upigaji kura.
Aidha, kamishna huyo amewakumbusha wanasiasa kuwa katika kila kinyang’anyiro cha kidemokrasia, lazima kuwe na mshindi na pia mshinde, akiwashauri kuanza kujitayarisha kwa matokeo yoyote badala ya kuchochea hisia kali.