Rais mteule wa Guinea: Kipaumbele changu ni kuleta umoja, utulivu na maendeleo
-
Rais mteule wa Guinea: Kipaumbele changu ni kuleta umoja, utulivu na maendeleo
Rais mteule wa Jamhuri ya Guinea, Mamady Doumbouya, ameahidi kufanyia kazi sana suala la kuleta umoja na mshikamano, utawala wa sheria na ustawi wa wananchi wote, katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
Doumbouya amesema hayo kwenye hotuba yake ya kwanza kwa taifa baada ya kushinda katika Uchaguzi Mkuu na amewashukuru wananchi wa Guinea kwa ukomavu wao, utulivu na hisia zao kali za uwajibikaji. Amesema kuwa, Uchaguzi Mkuu uliopita umeonesha uwezo wa nchi hiyo wa kuendeleza mchakato wake wa kisiasa kwa mujibu wa sheria na kwa kuheshimiwa taasisi husika.
"Hakuna washindi wala walioshindwa, bali leo kuna Guinea moja tu, iliyoungana na isiyogawanyika," amesema na kuwataka wananchi wote kusahau tofauti zao, kuimarisha umoja na kushiriki kwa pamoja katika miradi ya maendeleo ya taifa.
Doumbouya pia amesema kwamba, muhula wake mpya utaongozwa na sheria za kufanya kazi kwa bidii, kutomuonea muhali mtu pamoja na umoja na mshikamano. Pia amesema, kipaumbele kikubwa zaidi kitakuwa ni maendeleo ya kiuchumi na kuboresha maisha ya watu.
Vilevile ameahidi kuimarisha huduma za umma na kuendeleza mageuzi katika sekta muhimu kama vile elimu, afya na miundombinu, ili matunda ya maendeleo yawanufaishe raia wote.
Aidha amesema: "Serikali yangu itaendelea kudumisha mazungumzo na makundi yote ya kijamii, kuimarisha utulivu wa kitaifa, kukuza maridhiano ya kijamii na kuimarisha ushirikiano na nchi jirani pamoja na jumuiya ya kimataifa kwa msingi wa kuheshimiana."
Mahakama Kuu ya Guinea Jumapili jioni ilithibitisha matokeo ya mwisho ya uchaguzi wa rais wa Desemba 28, ikimtangaza Doumbouya kuwa mshindi kwa asilimia 86.72 ya kura.