Polisi wa Nigeria wakanusha ripoti za utekaji nyara kanisani huko Kaduna
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i135722-polisi_wa_nigeria_wakanusha_ripoti_za_utekaji_nyara_kanisani_huko_kaduna
Polisi wa Nigeria wamekanusha ripoti kwamba waumini walitekwa nyara makanisani katika jimbo la Kaduna siku ya Jumapili iliyopita, wakisisitiza kwamba hakuna shambulio kama hilo lililotokea.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jan 21, 2026 04:14 UTC
  • Kaduna, Nigeria
    Kaduna, Nigeria

Polisi wa Nigeria wamekanusha ripoti kwamba waumini walitekwa nyara makanisani katika jimbo la Kaduna siku ya Jumapili iliyopita, wakisisitiza kwamba hakuna shambulio kama hilo lililotokea.

Kamishna wa Polisi wa Kaduna, Alhaji Muhammad Rabiu, amezitaja ripoti hizo kuwa ni za uongo na kuwashutumu wahusika ambao hawakutajwa majina kwa kusambaza taarifa potofu ili kuchochea machafuko.

Ukanushaji huo umefuatia madai ya awali kutoka kwa afisa wa eneo la Kurmin Wali, ambaye aliiambia BBC kwamba watu wenye silaha  wamewateka nyara watu kadhaa waliokuwa wakihudhuria ibada kanisani.

Polisi ya Nigeria imesema hakuna ushahidi wowote unaounga mkono madai hayo. Kamishna huyo amewapa changamoto wanaotoa madai hayo kutoa majina na maelezo ya mwaathiriwa hata mmoja wa madai hayo.

Askari usalama wamlitumwa Kurmin Wali baada ya ripoti hizo kusambaa katika vyombo vya habari. Mwenyekiti wa serikali ya mtaa ya Kajuru, Dauda Madak, amesema maafisa wa serikali wamezungumza na viongozi wa jamii na wakazi wa eneo hilo na hawakupata dalili zozote za shambulio dhidi ya makanisa.

Kamishna wa usalama wa ndani wa Kaduna pia amesema viongozi wa kidini waliotembelea eneo hilo wamehitimisha kwamba taarifa zilizosambazwa mitandaoni hazikuwa sahihi.

Nigeria imeshuhudia ongezeko la utekaji nyara wa watu katika miaka ya hivi karibuni, huku magenge ya wahalifu yakiwalenga raia wa dini mbalimbali, mara nyingi kwa ajili ya kuomba kikomboleo.