Mahakama ya Ubelgiji yafungua tena kesi ya mauaji ya Patrice Lumumba
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i135728-mahakama_ya_ubelgiji_yafungua_tena_kesi_ya_mauaji_ya_patrice_lumumba
Familia ya shujaa wa uhuru wa Kongo, Patrice Lumumba, ilisema jana Jumanne kwamba inatumai kupata haki, huku mahakama ya Ubelgiji ikizingatia kumfungulia mashtaka mshukiwa pekee aliyebakia hai hadi sasa kuhusu mauaji ya mwaka 1961 ya Lumumba.
(last modified 2026-01-21T09:14:21+00:00 )
Jan 21, 2026 07:47 UTC
  • Patrice Lumumba
    Patrice Lumumba

Familia ya shujaa wa uhuru wa Kongo, Patrice Lumumba, ilisema jana Jumanne kwamba inatumai kupata haki, huku mahakama ya Ubelgiji ikizingatia kumfungulia mashtaka mshukiwa pekee aliyebakia hai hadi sasa kuhusu mauaji ya mwaka 1961 ya Lumumba.

Ndugu wa Lumumba wamekuwa wakishinikiza kwa miaka 15 iliyopita kile wanachosema ni uamuzi wa kisheria uliochelewa kwa muda mrefu kuhusu ushiriki wa maafisa wa Ubelgiji katika mauaji ya shujaa huyo wa Kongo na Afrika.

"Hatuwezi kurudisha wakati nyuma... lakini tunategemea mfumo wa haki wa Ubelgiji utafanya kazi yake na kutoa mwanga kuhusu historia," Yema Lumumba, mwenye umri wa miaka 33, mjukuu wa marehemu waziri mkuu wa Kongo, ameiambia AFP nje ya mahakama ya Brussels, kabla ya kesi hiyo kusikilizwa kwa faragha.

Yapata miaka 65 baada ya Lumumba kunyongwa na mwili wake kuyeyushwa na waasi katika asidi kwa msaada wa mamluki kutoka utawala wa zamani wa kikoloni wa Ubelgiji, ni afisa mmoja tu wa zamani wa Ubelgiji ambaye bado yuko hai kwa ajili ya kukabiliwa na mkono wa sheria.

Mtuhumiwa huyo ni Etienne Davignon mwenye umri wa miaka 93, ambaye aliwahi kuwa kamishna wa Ulaya. Davignon alikuwa mwanadiplomasia wa Ubelgiji wakati wa mauaji ya Lumumba.

Anatuhumiwa na waendesha mashtaka wa Shirikisho la Ubelgiji kwa kuhusika katika "kumzuilia na kumsafirisha Lumumba kimyume cha sheria" pamoja na "matendo ya kufedhehesha na kudhalilisha".

"Suala hili halihusu kulipiza kisasi, bali kuhusu kiu ya kupata maarifa," amesema Roland Lumumba, mmoja wa wana wa Patrice, kwa njia ya simu kutoka Kinshasa na kusisitiza kuwa: "Mamilioni ya watu wangependa kujua ukweli."

Mauaji ya Patrice Lumumba -- ambaye alikua waziri mkuu wa Kongo wakati wa uhuru mwaka 1960 -- ni mojawapo ya kurasa nyingi za giza katika historia mbaya ya ukoloni wa Ubelgiji katika kile kilichokuja kuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ya kisasa.

Familia yake inasema kulikuwa na "njama kubwa" iliyowahusisha maafisa wa Ubelgiji ili kumuua kiongozi huyo wa Kongo.