HRW: Hali ya haki za binadamu Kenya imeendelea kutia wasiwasi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i136310-hrw_hali_ya_haki_za_binadamu_kenya_imeendelea_kutia_wasiwasi
Ripoti mpya ya shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) inaonyesha kuwa, hali ya haki za binadamu nchini Kenya ilidorora mwaka uliopita, huku serikali ikikosolewa vikali kwa kukandamiza waandamanaji, wanaharakati, wanahabari na wakosoaji wa serikali.
(last modified 2026-02-06T06:21:33+00:00 )
Feb 06, 2026 06:21 UTC
  • HRW: Hali ya haki za binadamu Kenya imeendelea kutia wasiwasi

Ripoti mpya ya shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) inaonyesha kuwa, hali ya haki za binadamu nchini Kenya ilidorora mwaka uliopita, huku serikali ikikosolewa vikali kwa kukandamiza waandamanaji, wanaharakati, wanahabari na wakosoaji wa serikali.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, “hali ya haki za binadamu Kenya imeendelea kuwa ya kutia wasiwasi, huku serikali ikiendeleza msako mkali dhidi ya waandamanaji wanaodumisha amani”.

HRW imesema kuwa, maafisa usalama waliokuwa wamevaa mavazi ya kiraia walihusika katika visa vya utekaji nyara, ukandamizaji na kupotezwa watu waliotuhumiwa kuandaa au kuunga mkono maandamano ya kupinga serikali pamoja na wanaharakati wa mitandaoni.

Gazeti la Taifa Leo limenukuu ripoti hiyo ikieleza kuwa, “Serikali imefanya juhudi ndogo kuhakikisha uwajibikaji kwa ukiukaji huu na mengine mengi”, hali ambayo imeongeza hasira za umma dhidi ya serikali.

HRW inaeleza kuwa maandamano yaliendelea kushuhudiwa mwaka 2025 kutokana na sababu kadhaa, kama hasira za wananchi kuhusu nyongeza ya ushuru mwaka 2024 bila uwajibikaji wa matumizi ya fedha za umma.

HRW inasema kuwa polisi waliua angalau watu 31 wakati wa maandamano hayo, huku Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu nchini humo ikiripoti kuwa, watu 26 bado hawajulikani walipo tangu yajiri maandamano hayo.

Ripoti ya pamoja ya HRW na Amnesty International Kenya ya Novemba 2024, ilibaini kuwa “hakuna hata afisa mmoja wa polisi au afisa wa serikali aliyefunguliwa mashtaka kwa mauaji ya watu wasiopungua 31 wakati wa maandamano ya kulalamikia gharama ya maisha ya 2023”.