Ujenzi wa kituo cha Ebola cha Marekani nchini Kenya unaendelea kwa kasi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i139076-ujenzi_wa_kituo_cha_ebola_cha_marekani_nchini_kenya_unaendelea_kwa_kasi
Licha ya amri ya Mahakama Kuu ya Kenya ya kusimamisha ujenzi wa kituo cha karantini cha kuwapokea raia wa Marekani wanaoshukiwa kuwa na Ebola na maandamano ya Wakenya wenye hasira huko Nanyuki, ujenzi wa kituo hicho unaendelea kwa kasi ndani ya kambi ya jeshi ya Laikipia katikati mwa Kenya.
(last modified 2026-06-12T11:02:07+00:00 )
Jun 12, 2026 04:38 UTC
  • Maandamano ya kupinga ujenzi wa kituo cha Ebola cha Marekani nchini Kenya
    Maandamano ya kupinga ujenzi wa kituo cha Ebola cha Marekani nchini Kenya

Licha ya amri ya Mahakama Kuu ya Kenya ya kusimamisha ujenzi wa kituo cha karantini cha kuwapokea raia wa Marekani wanaoshukiwa kuwa na Ebola na maandamano ya Wakenya wenye hasira huko Nanyuki, ujenzi wa kituo hicho unaendelea kwa kasi ndani ya kambi ya jeshi ya Laikipia katikati mwa Kenya.

Picha za setilaiti zilizochambuliwa na kitengo huria cha Al Jazeera zilizochukuliwa na Planet Labs PBC kati ya Mei 27 na Juni 8, 2026, zimeonyesha kuwepo kasi kubwa katika kazi ya maandalizi ya eneo hilo kwa ajili ya kituo cha karantini ambacho Washington inasema kinatayarishwa kwa ajili ya Wamarekani ambao wanaweza kuwa katika hatari ya kuambukizwa virusi vya Ebola.

Ulinganisho wa picha hizo unaonyesha kwamba eneo hilo lilibadilika ndani ya siku chache kutoka eneo tupu hadi eneo lililosafishwa na kusawazishwa, huku mahema na vifaa vya uwanjani vikionekana ndani ya mipaka ya kambi hiyo.

Jumla ya eneo lililosafishwa ndani ya mipaka ya eneo hilo inakadiriwa kuwa takriban mita za mraba 40,000, sawa na takriban ekari 10.

Picha hizo hazionyeshi asili ya kila kituo ndani ya eneo hilo au kiwango chake cha maandalizi tu, bali zinaonyesha pia mabadiliko ya haraka katika hali ya ardhi katika kipindi cha chini ya wiki mbili, jambo ambalo linaimarisha dalili za kuendelea kazi ya ujenzi licha ya utata unaozunguka mradi huo.

Washington inadai kuwa kituo hicho ni cha karantini na ufuatiliaji wa uwanjani wa Wamarekani ambao wanaweza kuwa katika hatari ya kuambukizwa virusi vya Ebola wakati wakifanya kazi katika maeneo ya mlipuko, hasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Uganda, badala ya kuwasafirisha moja kwa moja hadi Marekani.

Mahakama Kuu ya Kenya ilitoa uamuzi wa kuongeza muda wa kusimamishwa mradi huo kwa wiki 3 zaidi, baada ya hapo awali kuusitisha kutokana na kesi iliyowasilishwa na shirika la kutetea haki za binadamu.

Jaji Patricia Nyaundi alitoa maagizo hayo baada ya kundi la kutetea haki kupinga mradi huo, likisema kuwa unazua masuala ya kikatiba na ya maslahi ya umma yanayohitaji mapitio ya kimahakama.

Licha ya uamuzi huo wa mahakama, vyanzo vya kidiplomasia na afisa mmoja wa Marekani viliripoti kwamba ndege za kijeshi za nchi hiyo zimeendelea kusafirisha wafanyakazi na vifaa hadi eneo hilo katika siku za hivi karibuni, ikionyesha kwamba maandalizi yalikuwa yakiendelea.

Jumanne wiki hii Polisi wa Kenya walitumia gesi ya kutoa machozi dhidi ya raia waliokuwa wakiandamana huko Nanyuki kupinga kuanzishwa kituo cha karantini cha Marekani ndani ya kambi ya kijeshi ili kuwapokea raia wa Marekani wanaoshukiwa kuwa na Ebola.

Maandamano hayo yalifuatia maandamano kama hayo mapema mwezi huu ambayo yalisababisha vifo vya watu wawili katika mji wa Nanyuki, baada ya polisi kuwafyatulia risasi mamia ya waandamanaji waliokuwa wamekusanyika karibu na kambi ya Laikipia.

Mbali na utata unaouhusu masua ya kikatiba, vilevile kauli ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, kuwa Marekani haitawaruhusu kuingia nchini humo waathirika au washukiwa wa ugonjwa wa Ebola na kwamba watatibiwa katika nchi nyingine imewakasirisha sana Wakenya wanaoona kwamba nchi yao inatumiwa na Marekani kama jaa la taka.