Africa CDA: Mlipuko wa ugonjwa wa Ebola DRC unaenea kwa kasi ya kutisha
-
Mlipuko wa Ebola unaenea kwa kasi ya kutisha katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
Mkurugenzi Mkuu wa Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa barani Afrika (Africa CDC) ametoa wito wa kuchukuliwa kwa hatua za haraka ili kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa Ebola unaoendelea kuenea kwa kasi ya kutisha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Ameonya kuwa ikiwa mataifa hayatachukua hatua kuzuia kuenea virusi hivyo sasa, “mlipuko wa sasa utageuka kuwa mbaya zaidi ambao dunia imewahi kuushuhudia.”
Siku sitini na tano tangu kuanza kwa mlipuko huu wa sasa, idadi ya visa vilivyothibitishwa ilifikia 2,423 mnamo Jumanne, huku vifo vikifikia 967 tangu mlipuko huo kutangazwa Mei 15. Hayo bni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya ya DRC.
Kiwango cha vifo vinavyotokana na ugonjwa huo kimesimama kwa asilimia 39.9, wakati kiwango cha ufuatiliaji wa watu waliogusana na wagonjwa kikiwa ni asilimia 81.1.
Jean Kaseya, Mkurugenzi Mkuu wa Africa CDC, amesema katika ujumbe wake kwenye mtandao wa X kwamba: “Mlipuko wa Ebola unaongezeka kwa kasi ya kutisha. Ni lazima tuchukue hatua sasa. Ikiwa hatutaumaliza leo, huu utakuwa mlipuko mbaya zaidi kuwahi kurekodiwa duniani. Huu si wakati wa kusita. Ni lazima tuhamasishe kila rasilimali inayopatikana, tuimarishe mwitikio katika maeneo yaliyoathirika, na tuukomeshe mlipuko huu kabla ya maisha zaidi kupotea.”
Virusi hivyo vimeathiri majimbo matano, ikiwa ni pamoja na Haut-Uele, Ituri, Kivu Kaskazini, Kivu Kusini, na Tshopo.
Ituri inasalia kuwa kitovu cha janga hilo linalosababishwa na aina ya virusi ya Bundibugyo, huku maambukizi yakiendelea kusambaa kwa kasi.
Kaseya amesisitiza umuhimu wa kukumbuka kuwa nyuma ya kila takwimu, kuna mtu, familia, na jamii inayoteseka.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), idadi ya maeneo ya afya yaliyoathirika imeongezeka kutoka 36 hadi 42 ndani ya wiki moja iliyopita.