Uasi na machafuko katika mji mkuu wa Kongo DR, Kinshasa
(last modified Sat, 24 Sep 2016 11:45:43 GMT )
Sep 24, 2016 11:45 UTC
  • Uasi na machafuko katika mji mkuu wa Kongo DR, Kinshasa

Kuendelea ghasia na machafuko kati ya waandamanaji na askari usalama nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kumeitia wasiwasi jamii ya kimataifa.

Katika hali ambayo wapinzani wa serikali ya Kinshasa wanasema idadi ya watu waliouawa hivi karibuni huko Kinshasa mji mkuu wa Kongo DR hawapungui 50, duru za serikali kwa upande wake zimetangaza kuwa  watu 17 wameuawa huko Kinshasa. Kushtadi machafuko katika mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kumemfanya Vital Kamerhe, mwakilishi wa Muungano wa vyama vya upinzani nchini humo asisitize kuakhirisha kushiriki katika mazungumzo ya kitaifa ikiwa ni kulalamikia ghasia za hivi karibuni katika mji mkuu Kinshasa zilizosababisha umwagaji damu. 

Ghasia za Kinshasa zilizosababisha vifo vya makumi ya watu

Hii ni mara ya pili  ambapo Vital Kamerhe mjumbe wa wapinzani kwenye mazungumzo ya kitaifa ya Kongo anaakhirisha kuhudhuria kikao cha pamoja kati yao na wawakilishi wa serikali, tangu kuanza mazungumzo hayo huko Kinshasa. Wiki mbili zilizopita Kamerhe alikataa pia kuhudhuria mazungumzio hayo kwa maelezo kwamba matokeo ya mazungumzo kati yao na wawakilishi wa serikali hayatakuwa na faida yoyote. Mazungumzo hayo ya kitaifa  yameanza tangu tarehe Mosi mwei huu lengo likiwa ni kutanzua mgogoro wa kisiasa wa Kongo.Katika hali ambayo weledi wa mambo walitaraji kuwa kikao cha Kinshasa kitazaa matunda ili kuhitimisha mkwamo wa kisiasa huko Kongo, lakini hivi sasa uasi, vitendo vya wizi na  uporaji na machafuko vimeenea katika mji mkuu wote wa nchi hiyo.

Wazushaji ghasia na wafanya maandamano wanamtaka Rais Joseph Kabila ang'atuke madarakani ifikapo Disemba 20 mwaka huu, ambapo duru yake ya pili ya urais inamalizika. Pamoja na hayo yote, Joseph Kabila na waitifaki wake katika chama tawala wameakhirisha muda wa kisheria wa kufanyka uchaguzi yaani tarehe 27 Novemba mwaka huu kwa sababu zisizo na msingi.Vyama vya upinzani Kongo vinaona kuwa, Rais Kabila anafanya kila awezalo kuakhirisha uchaguzi wa Rais ili asalie madarakani. Pamoaj na kuwa haujabaki muda mrefu hadi kufikia tarehe 20 Disemba, lakini Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Kongo bado haijatangaza tarehe rasmi ya kufanyika uchaguzi mpya nchini humo.

Sababu hizo ziliufanya Muungano wa wapinzani uwatolee wito wakazi wa Kinshasa kuandamana mitaani Jumatatu iliyopita kulalamikia kuakhirishwa uchaguzi mpya huko Kongo; maandamano ambayo yalisababisha ghasia za umwagaji damu kati ya raia na polisi wa kuzuia fujo. Muungano wa vyama vya upinzani kwa jina la " G-7"  umeundwa chini ya uongozi wa  chama kikuu cha upinzani cha Umoja kwa Ajili ya Demokrasia na Maendeleo cha mzee Etienne Tshisekedi mwanasiasa mtajika wa Kongo.Tshisekedi anajitambua kuwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tangu kufanyika uchaguzi wa rais nchini mwaka 2011 na hakuwa tayari kivyovyote kukubali ushindi wa  Joseph Kabila.

Mwanasiasa mkongwe wa Kongo mzee Etienne Ttshisekedi

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa chimbuko la ghasia za hivi majuzi huko Kongo linahusiana na mikwaruzano ya kiuchaguzi ya miaka mitano iliyopita. Wakati huo mzee Etienne Tshisekedi  kamwe hakuwa tayari kukubali kwamba Joseph Kabila ni Rais halali wa Kongo. Kwa msingi huo, mwanasiasa huyo ameshindwa  kukitambua rasmi kikao cha mazungumzo ya kitaifa ya nchi hiyo pia kinachofanyika katika mji mkuu Kinshasa. Mahakama ya katiba ya Kongo imetangaza kuwa Kabila  anaweza kuendelea kusalia uongozini madhali uchaguzi mpya haujafanyika, licha ya katiba ya nchi hiyo kueleza kuwa Joseph Kabila haruhusiwi kugombea  urais kwa mara ya tatu.