Mabaharia 26 waliotekwa nyara Somalia miaka 5 iliyopita waachiliwa huru
Mabaharia wapatao 26 wa Asia waliokuwa wakishikiliwa mateka na maharamia wa Somalia yapata miaka mitano sasa wameachiliwa huru.
Mabaharia hao kutoka China, Ufilipini, Cambodia, Indonesia, Vietnam na Taiwan walitkwa nyara na maharamia wa Somalia Machi mwaka 2012 na kushikiliwa mateka tangu wakati huo.
Imeelezwa kuwa, kwa sasa mabaharia hao wako mikononi mwa mamlaka za jimbo la Galmudug lililoko katikati mwa Somalia na kwamba, kunafanyika taratibu za kuwasafirishia nchini kwao kwa kutumia ndege ya misaada ya Umoja wa Mataifa.
Mnamo Machi 26 mwaka 2012 maharamia wa Somalia waliivamia meli ya FV Naham-3 ilipokuwa inaeleka Ushelisheli.
Maharamia hao wa Somalia waliiteka vyara meli hiyo na mabahari waliokuwemo ndani yake. Takriban mwaka mmoja baadaye, meli hiyo
ilizama. Mateka walifikishwa pwani ya Somalia na kushikiliwa mateka.
Tofauti na visa vingine, hapakuwa na kitita cha pesa kilichowasilishwa kutoka kampuni iliyomiliki meli hiyo. Lakini hatimaye majadiliano ya miaka kadhaa ya kundi dogo la watu wanaojitahidi kuwaokoa mabaharia waliosahauliwa yamezaa matunda.
Maharamia wa Kisomalia wamekuwa wakiziteka nyara mara kwa mara meli na mabaharia na kisha kudai kikomboleo cha kuachilia huru meli hizo la mabaharia wake. Maelfu ya meli hupita kwenye maji ya Ghuba ya Aden kila mwaka kupitia mfereji wa Suez. Harakati za maharamia katika Ghuba ya Aden zimekuwa zikishadidi kila uchao licha ya wanamaji wa kigeni kuendelea kupiga doria katika eneo hilo.