Sep 17, 2023 04:39 UTC
  • Jumapili, tarehe 17 Septemba, 2023

Leo ni Jumapili tarehe Mosi Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1445 Hijria sawa na Septemba 17 mwaka 2023.

Siku kama ya leo miaka 1445 iliyopita, Mtume Muhammad SAW alianza Hijra yake ya kuhama Makka na kuelekea Madina, ikiwa imepita miaka 13 tokea alipobaathiwa na kupewa Utume. Mtume wa Allah alihama Makka kutokana na kushadidi vitimbi vya washirikina wa mji huo ambao walikusudia kumdhuru na kumuua wakati wa usiku akiwa amelala nyumbani kwake. Imam Ali AS alijitolea mhanga, kwa kuamua kulala kwenye kitanda cha Mtume, ili maadui wasitambue kwamba Mtume wa Allah ameondoka mjini Makka. Hijra ya Mtume SAW na matukio ya baada yake yalikuwa na umuhimu mkubwa katika ustawi na maendeleo ya Uislamu kiasi kwamba lilitambuliwa kuwa mwanzo wa kalenda ya Kiislamu. Ni vyema kukumbusha hapa kuwa Mtume (saw) ndiye aliyekuwa wa kwanza kutumia hijra yake kama mwanzo wa kalenda ya Kiislamu kwani barua zote zilizoandikwa na mtukufu huyo kwa wakuu wa makabila na shakhsia maarufu alizisajili kwa kalenda hiyo.

Tarehe Mosi Rabiul Awwal miaka 1380 iliyopita, ilianza harakati ya Tawwabin kwa lengo la kulipiza kisasi cha kuuawa shahidi Imam Hussein AS pamoja na wafuasi wake watiifu. Awali, watu wa Kufa walimuomba Imam Hussein AS aelekee mjini humo kwa lengo la kuongoza harakati dhidi ya utawala wa kidhalimu wa Yazid bin Muawiya lakini alizingirwa njiani na jeshi la mtawala dhalimu, Yazid bin Muawiya, na kuuawa shahidi. Tawwabin ni kundi la watu wa Kufa ambalo lilijuta kwa kushindwa kutekeleza ahadi yake na kumuacha Imam Hussein na wafuasi wake wachache peke yao wapambane na majeshi ya Yazid. Kwa minajili hiyo watu hao walitubia makosa yao na kuamua kuanzisha harakati ya kulipiza kisasi wakiongozwa na Sulaiman bin Sorad dhidi ya jeshi la Yazid. Kundi hilo lilipigana kishujaa na jeshi la Yazid na wengi kati ya wapiganaji wake wakauawa shahidi. 

Siku kama ya leo miaka 75 iliyopita, aliaga dunia Emil Ludwig mwandishi wa wasifu wa Kijerumani.

Alizaliwa 1881 katika mji wa Breslau nchini Ujerumani ambao leo hii ni sehemu ya ardhi ya Poland. Alipata umashuhuri katika nusu ya pili ya karne ya 19 baada ya kuandika wasifu wa Otto Van Bismarck Kansela wa wakati huo wa Ujerumani, kiongozi wa zamani wa Russia Joseph Stalin, Beethoven na rais wa zamani wa Marekani Franklin Roosevelt.

Wakati wa Vita vya Pili vya Dunia Ludwig alikuwa mwandishi wa habari aliyepata nafasi ya kufanya mahojiano na watawala waliokuwa na satua na ushawishi mkubwa katika kipindi hicho kama Franklin Delano Roosevelt, Winston Churchil na Joseph Stalin.

Emil Ludwig

Tarehe 17 Septemba miaka 62 iliyopita aliuawa waziri mkuu wa zamani wa Uturuki, Adnan Menderes.

Alizaliwa mwaka 1899 na kupata elimu katika taaluma ya sheria. Alijiunga na harakati za kisiasa akiwa bado kijana na alishika hatamu za uongozi nchini Uturuki kama waziri mkuu mwaka 1950. Menderes ambaye alikuwa akifuata siasa za sera za kimarekani, alituma vikosi vya jeshi kushambulia Wakurdi wa nchi hiyo, suala ambalo liliwakasirisha sana wasomi na wanafikra wengi nchini Uturuki. Mwaka 1957 alichaguliwa tena kuwa Waziri Mkuu wa Uturuki na kukandamiza maandamano ya wanafunzi wa vyuo vikuu waliokuwa wakipinga utawala wake na kudai marekebisho ya kisiasa. Mwaka 1960 Adnan Menderes aliondolewa madarakani katika mapinduzi ya kijeshi na kufikishwa mahakamani ambapo alihukumiwa kifo kwa kupatikana na hatia ya kuua wanafunzi wa vyuo vikuu, kukiuka katiba ya nchi na kuwa na mahusiano haramu.

Usiku wa kutekelezwa hukumu ya kifo, Menderes alifanya jaribio la kujiua lakini madaktari waliwahi kuokoa maisha yake. Hatimaye tarehe 17 Septemba, Adnan Menderes alinyongwa akiwa na umri wa miaka 62. 

Adnan Menderes

Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita sawa na tarehe 17 Septemba 1982, wanamgambo wa Kikristo wenye misimamo ya kufurutu ada wa kundi la Mafalanja wakipata himaya ya askari wa utawala haramu wa Israel walifanya mauaji makubwa katika kambi za wakimbizi wa Kipalestina huko Sabra na Shatila nchini Lebanon.

Ilikuwa Juni mwaka 1982 wakati askari 150,000 wa utawala haramu wa Israel walipoishambulia Lebanon na kuukalia kwa mabavu baada ya kuwalazimisha wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO kuondoka Beirut. Kwa amri ya Menachem Begin Waziri Mkuu wa wakati huo wa Israel na Ariel Sharon Waziri wa Vita wa utawala huo, tarehe kama ya leo askari wa Israel waliizingira kambi za Sabra na Shatila kisha mafalanja wa Lebanon wakaanza kufanya mauaji ya kinyama dhidi ya wakimbizi wa Kipalestina waliokuwamo katika katika kambi hizo. Wapalestina wasiokuwa na hatia 3,300 waliuawa shahidi katika mashambulio hayo.  ***

Tags