Lugha ya Kifarsi inafunzwa katika vyuo vikuu 200 duniani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i43558-lugha_ya_kifarsi_inafunzwa_katika_vyuo_vikuu_200_duniani
Lugha ya Kifarsi, ambayo ni lugha rasmi na ya taifa nchini Iran, hivi sasa inafunzwa katika zaidi ya vyuo vikuu 200 duniani.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 24, 2018 03:16 UTC
  • Lugha ya Kifarsi inafunzwa katika vyuo vikuu 200 duniani

Lugha ya Kifarsi, ambayo ni lugha rasmi na ya taifa nchini Iran, hivi sasa inafunzwa katika zaidi ya vyuo vikuu 200 duniani.

Ridha Murad Sahrai, Mkuu wa Kituo cha Kufunza Lugha ya Kifarsi nchini Iran, ameyaeleza hayo katika kongamano la 'Hali ya Lugha ya Kifarsi Duniani' na kuongeza kuwa: "Lugha ya Kifarsi inafunzwa katika vituo vya vyuo vikuu vya bara Asia na nchi zinazopakana na Iran kama vile Kirghizstan na Uturuki, Iraq, Pakistan Russia, Turkmenistan, Iraq na Qatar pamoja na nchi kama vile Lebanon, Syria , China India, na Bangladesh. "

Aidha amesema katika Kituo cha Kufunza Lugha ya Kifarsi katika mji mkuu wa Pakistan, Islamabad, kuna nakala 20,000 za vitabu vya kale vya maandishi ya Kifarsi ya Iran na Pakistan. Amesema nchini India kuna zaidi ya maeneo 40 ya kufunza lugha ya Kifarsi katika viwango vya shahda za uzamili na uzamivu.

Halikadhalika amesema katika miji mikubwa ya Ulaya kama vile Athens, Stockholm, Berlin, Belgrade, Paris, Rome, Sofia, London, Madrid, Vienna na Warsaw, lugha ya Kifarsia inafunzwa katika vyuo vikuu au katika vituo maalum. Bw. Ridha Murad Sahrai amesema lugha ya Kifarsi pia inafunzwa katika vituo kadhaa  barani Afrika na Australia. Anasema wengi wanaojifunza lugha ya Kifarsi wanafanya hivyo kutokana na kuwa wanasomea taaluma kama vile historia na utaalamu wa ulimwengu wa mashariki. Aidha amesema kuna wale wanaosoma lugha ya Kifarsi kwa malengo ya kitiba, kidini, kijeshi, kisiasa, kibiashara na kitalii.