Askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Mataifa CAR walaumiwa kwa udhaifu
Raia wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wamekosoa vikali udhaifu wa askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Mataifa ndani ya nchi hiyo.
Jumatatu ya jana wakazi wa mji mkuu wa nchi hiyo, Bangui walimiminika barabarani kuzuia safari za magari katika maeneo tofauti na kusimamisha shughuli za biashara mjini humo. Mratibu wa jumuiya za kiraia nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati amesema kuwa, majukumu ya askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini humo MINUSCA, yako wazi, na kwamba lengo lao kuu ni kupunguza makundi ya wabeba silaha; hata hivyo na licha ya idadi kubwa ya askari hao, raia wamekuwa wakiuawa na makundi hayo kila siku.
Inafaa kuashiria kuwa, kikosi cha askari wa MINUSCA, kinaundwa na askari na polisi wa Umoja wa Mataifa zaidi ya elfu 10. Kabla ya hapo, jumuiya za kiraia nchini humo zilikuwa zimeitisha maandamano makubwa kwa ajili ya kulalamikia utendaji dhaifu wa askari hao katika kukabiliana na makundi ya wabeba silaha nchini humo.