HRW: Rais wa Gambia anawatesa wapinzani na wakosoaji wake
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i18703-hrw_rais_wa_gambia_anawatesa_wapinzani_na_wakosoaji_wake
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch linamtuhumu Rais wa Gambia Yahya Jammeh kuwa anawakandamiza na kuwatesa wapinzani na wakosoaji wake na kwamba yumkini uchaguzi mkuu ujao wa Disemba Mosi usiwe huru na wa haki.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 03, 2016 03:54 UTC
  • HRW: Rais wa Gambia anawatesa wapinzani na wakosoaji wake

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch linamtuhumu Rais wa Gambia Yahya Jammeh kuwa anawakandamiza na kuwatesa wapinzani na wakosoaji wake na kwamba yumkini uchaguzi mkuu ujao wa Disemba Mosi usiwe huru na wa haki.

Ripoti ya kurasa 43 ya Human Rights Watch imesema Rais wa Gambia ameviwekea mbinyo vyama vya upinzani sambamba na kuvinyima nafasi ya kufanya kampeni zao wakati huu ambapo uchaguzi wa rais unakaribia.

Babatunde Olugboji, Naibu Mkurugenzi wa Mipango wa shirika hilo amesema mbali na kuvikandamiza vyama vya upinzani, Jammeh anatumia vyombo vya habari vya dola na fedha kutoka hazina ya taifa katika kampeni zake.

Ousainou Darboe, kiongozi wa upinzani Gambia

Mwezi Julai mwaka huu, kiongozi wa upinzani nchini Gambia Ousainou Darboe alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela, pamoja na watu wengine 18 baada ya kupatikana na makosa kadhaa yanayohusiana na maandamano yaliyofanywa dhidi ya serikali mwezi Aprili. Makumi ya raia walitiwa mbaroni nchini Gambia kwa kushiriki maandamano hayo ya kumpinga Rais Yahya Jammeh wa nchi hiyo.

Maandamano huwa nadra sana kufanyika  nchini Gambia, ambayo imetawaliwa na Rais Yahya Jammeh tangu achukue madaraka kupitia mapinduzi ya kijeshi 1994. Mashirika mbalimbali ya kutetea haki za binadamu na Umoja wa Mataifa yamelaani hatua hiyo. 

Rais Yahya Jammeh wa Gambia

Hii ni katika hali ambayo, hivi karibuni Gambia ilijiunga na nchi kadhaa za Afrika zilizotangaza azma yao ya kujiondoa katika Mkataba wa Roma uliobuni Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC.