Feb 18, 2026 03:20 UTC
  • Jumatano, 18 Februari, 2026

Leo ni Jumatano 29 Sha'ban 1447 Hijria sawa na 18 Februari 2026.

Siku kama ya leo miaka 1228 iliyopita inayosadifiana na 29 Sha'ban 219 Hijria, alifariki dunia Ibn Naeem mtaalamu wa elimu ya Hadithi, faqihi na mpokezi wa riwaya za kihistoria.

Msomi huyo alizaliwa nchini Iraq na anahesabiwa kuwa mmoja wa wapokezi wa kutegemewa sana wa Hadithi kati ya maulamaa wa Kiislamu. 

Kitabu "Al-Salat" ni mojawapo ya vitabu vya Abu Naeem. Ibn Nadim, mwanahistoria maarufu alimhusisha na vitabu vingine viwili, "Al-Manasik" na "Masailul -Fiqh" kuhusu masuala ya sheria na adabu za kidini.***

Tarehe 29 Sha'ban miaka 1129 iliyopita aliaga dunia

Ibn Mundhir faqihi, mfasiri na mpokeaji Hadithi wa Kiislamu.

Ibn Mundhir alijifunza masomo ya fiqih na Hadithi kwa wasomi watajika wa zama zake. Aliishi katika mji wa Makka hadi mwisho wa maisha yake baada ya kuwasili mjini humo kwa lengo la kuzidisha elimu na maarifa ya kidini.

Msomi huyo wa Kiislamu aliandika vitabu kadhaa akiwa Makka. Kitabu alichokipa jina la al Ashraaf ni moja ya vitabu vya msomi huyo ambacho ndani yake ameonyesha kipawa na elimu aliyokuwanayo katika taaluma ya Hadithi. 

 ******

Miaka 462 iliyopita katika siku kama hii ya leo, Michelangelo di Lodovico Buonarroti, mchongaji wa sanamu, msanifu majengo na malenga mkubwa wa Kiitalia aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 89.

Michelangelo alizaliwa mwaka 1475 na kuanza kujishughulisha na uchoraji na kuchonga sanamu licha ya upinzani wa baba yake. Malenga huyo wa Kiitalia alionyesha kipaji chake haraka katika uwanja wa uchoraji, uchongaji sanamu na usanifu majengo.

Uchongaji wa sanamu za Manabii Isa na Musa huko Italia ni moja kati ya kazi kubwa za kisanaa zilizofanywa na Michelangelo katika zama zake hizo.   ****

Siku kama ya leo miaka 192 iliyopita, vikosi vya utawala wa kikoloni wa Ufaransa ambavyo vilianza kuikalia kwa mabavu Algeria mwaka 1830, vilishindwa vibaya na wapiganaji wa Amir Abdelkader al-Djezairi, kiasi kwamba theluthi moja ya askari wa Ufaransa waliuawa na nusu nyingine ya waliobakia hai walikamatwa mateka.

Wakati huo Wafaransa ambao ndio ilikuwa mara yao ya kwanza kupata hasara kubwa ya namna hiyo barani Afrika, waliamua kuomba suluhu ili kujipanga upya na kukusanya nguvu. Hata hivyo Amir Abdelkader al-Djezairi alikataa ombi hilo, hadi baada ya kupita karibu miaka miwili na kuikomboa ardhi yote ya Algeria kutoka mikononi mwa Wafaransa hao wavamizi.

Miaka kadhaa baadaye Ufaransa iliweza kuidhibiti tena nchi hiyo baada ya kuongeza askari na zana za kijeshi sambamba na kuwatumia baadhi ya viongozi wasaliti wa makabila ndani ya Algeria.  ***

Katika siku kama ya leo miaka 100 iliyopita, askari wa Ufaransa na Uhispania, walivunja mapambano ya wapiganaji wa Morocco chini ya uongozi wa Abdel-Karim Rifi, na shujaa huyo Muislamu akapelekwa uhamishoni kusini mwa Afrika. 

Abdel-Karim Rifi alianzisha mapambano yake sambamba na kuanza uvamizi wa Uhispania katika sehemu ya ardhi ya Morocco hapo mwaka 1912. Hata hivyo na licha ya mkoloni huyo kuwa na nguvu kubwa na kutekeleza mauaji ya umati dhidi ya raia wa Morocco wasio na hatia, mwaka 1921 wapiganaji wa Abdel-Karim Rifi walipata ushindi mkubwa kiasi cha kuyafanya baadhi ya maeneo ya nchi hiyo kutangaza Jamhuri.

Wafaransa nao ambao walikuwa wakiyadhibiti baadhi ya maeneo ya nchi hiyo walipatwa na hofu kufuatia ushindi wa wananchi dhidi ya Wahispania na mwanzoni mwa mwaka 1924 walianzisha hujuma kubwa dhidi ya wanamapambano hao. Jeshi la Ufaransa chini ya Jemadari Philippe Pétain ambalo mwanzoni lilishindwa vibaya na wanamupambano wa Morocco, mwezi Februari 1926 katika siku kama ya leo liliwashinda wapiganaji wa Abdel-Karim Rifi baada ya kupata msaada wa kijeshi na kutekeleza jinai kubwa dhidi ya raia wa Morocco. Kwa utaratibu huo Ufaransa ikaweza kuendeleza ukoloni wake nchini Morocco.    ****

Siku kama ya leo miaka 61 iliyopita yaani tarehe 18 mwezi Februari mwaka 1965, Gambia ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza.

Uingereza ilianza kuikoloni Gambia mwaka 1588 na kupora rasilimali za nchi hiyo kwa karibu karne nne.

Mwaka 1963, Uingereza iliipatia Gambia mamlaka ya ndani baada ya kudhoofika kisiasa na kiuchumi kutokana na Vita vya Pili vya Dunia na kushindwa kuendesha makoloni yake. Hatimaye ilipofika mwaka 1965 Gambia ilipatia uhuru wake.

****

Miaka 59 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia mwanafizikia na mtengenezaji wa bomu la atomiki wa Marekani, Robert Oppenheimer.

Kabla ya Vita vya Pili vya Dunia mtaalamu huyo alifanya utafiti kuhusiana na jinsi ya kupasua atomu na kupata nishati ya nyuklia. Wakati wa vita hivyo alipewa wadhifa wa kusimamia kitengo cha utafiti katika Wizara ya Vita ya Marekani na chini ya usimamizi wake yakatengenezwa mabomu matatu ya kwanza ya nyuklia.

Hata hivyo, wakati Marekani ilipoishambulia Japan kwa mabomu ya nyuklia mwaka 1945, makumi ya maelfu ya watu wasio na hatia waliuawa katika kipindi kifupi, hali iliyomfanya Oppenheimer kujutia kitendo chake hicho na akatoa wito wa kutumiwa nishati ya atomiki katika masuala ya amani.     ****