Wito wa kuvumiliana kati ya serikali na wapinzani wa Kongo DR
Mkuu wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ameitolea mwito serikali na wapinzani nchini humo kuvumiliana.
Maman Sambo Sidikou ameitaka serikali ya Kinshasa iheshimu haki ya wapinzani wa kisiasa ya kufanya maandamano ya amani kama haki ya msingi ya kila mtu.
Wakati huo huo Maman Sidikou amesema idadi ya askari jeshi wa Kofia Bluu wa Umoja wa Mataifa imeongezwa huko Kinshasa mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ili kuwalinda raia na kuwasadia polisi wakati wa kufanyika maandamanao na iwapo kutatokea ghasia.
Itakumbukwa kuwa polisi ya Kongo imepiga marufuku maandamano ya aina yoyote ya kisiasa kufuatia kuongezeka mivutano ya kisiasa nchini humo katika siku za hivi karibuni katika miji mbalimbali ya ya nchi hiyo yaliyoambatana na ghasia na machafuko. Upinzani wa kisiasa umeongezeka Kongo baada ya uamuzi wa Rais Joseph Kabila wa kutaka kubakia madarakani baada ya kumalizika kipindi cha uongozi wake. Wapinzani nchini Kongo wanamtaka Rais Kabila aondoke madarakani muda wake wa kuwepo uongozini utakapomalizika na uchaguzi wa rais ufanyike mwakani. Hata hivyo kulingana na uamuzi uliotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada ya makubaliano yaliyofikiwa katika mazungumzo ya kitaifa, uchaguzi wa Rais umepangwa kufanyika mwaka 2018. Wapinzani wanasema kuwa, Kabila kama walivyo baadhi ya viongozi wa nchi za Kiafrika, anadhamiria kung'ang'ania hatamu za uongozi hatua ambayo ni kinyume na katiba na misingi ya demokrasia.
Maamuzi na hatua zote zilizochukuliwa hivi karibuni na serikali ya Joseph Kabila zimekuwa chanzo na sababu ya maandamano dhidi ya serikali. Kupamba moto malalamiko hayo kulisababisha mapigano makali kati ya wafuasi wa upinzani na polisi na kuchomwa moto majengo ya serikali katika mitaa ya mji Kinshasa. Ghasia hizo zilienea pia katika miji mingine ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa kadiri kwamba, makumi ya watu waliuliwa na wengine kujeruhiwa.
Pamoja na hayo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inahitajia kudumisha amani na utulivu hususan katika kipindi cha sasa ambapo nchi hiyo iko katika mivutano na hitilafu kubwa za ndani.
Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imeripoti mamia ya kesi za ukiukwaji wa haki za binadamu katika mwezi Septemba mwaka huu nchini humo. Hali hiyo imekifanya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Kongo MINUSCA kuchukua maamuzi kadhaa katika uwanja huo ikiwa ni pamoja na kuzidisha idadi ya askari wake katika jiji la Kinshasa.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pia limetangaza kwamba tarehe 11 mwezi huu ujumbe wa watu kadhaa utaelekea Kinshasa kufanya mazungumzo na viongozi wa serikali ya Congo, viongozi wa vyama na makundi ya upinzani na wawakilishi wa taasisi za kiraia kuhusu amani ya Kongo.
Kwa msingi huo wito uliotolewa na Umoja wa Mataifa kwa serikali na wapinzani huko Kongo DR na kuzitaka pande hizo kuvumiliana unahesabiwa kuwa ni katika juhudi za kurejesha utulivu wa kisiasa nchini humo.