Nov 11, 2016 04:38 UTC
  • Asasi za Kiafrika zasisitiza ulazima wa kutekelezwa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi

Asasi za Kiafrika zinazoshiriki katika mkutano wa 22 wa mabadiliko ya tabianchi nchini Morocco zimesisitiza juu ya udharura wa kutekelezwa vipengee vya mkataba wa mabadiliko ya tabianchi vilivyopasishwa katika mkutano wa Paris, Ufaransa.

Hayo yamesisitizwa katika mkutano wa mabadiliko ya tabianchi unaoendelea kufanyika nchini Morocco ambao moja ya malengo yake ni kuchunguza mwenendo wa utekelezwaji wa makubaliano ya mkutano wa Paris, Ufaransa uliofanyika Disemba mwaka  uliopita.

Taasisi za Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Kamisheni ya Uchumi ya Afrika, Benki ya Ustawi ya Afrika na asasi inayojuliakana kama ushiriki mpya kwa ajili ya ustawi Afrika jana zilikutana pambizoni mwa mkutano huo nchini Morocco na kusisitiza juu ya udharura wa kutekelezwa vipengee vilivyopasishwa katika mkutano uliopita.

Baadhi ya washiriki wa mkutano wa mabadiliko ya tabianchi nchini Morocco

Asasi hizo zimesisitiza mwishoni mwa mkutano wao kwamba, kuna haja ya kuweko umoja na mshikamano baina ya nchi za Kiafrika na kuundwa kambi ya pamoja kwa ajili ya kushiriki katika mazungumzo ya kimataifa ili kutetea maslahi ya bara la Afrika katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Inatarajiwa kuwa, viongozi na maafisa wa nchi 54 za Kiafrika ambao wataendelea kushiriki katika kikao hicho cha Morocco hadi Jumatano ijayo watachukua maamuzi ya pamoja kuhusiana na suala na changamoto za mabadiliko ya tabianchi barani Afrika.

Mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi unaofanyika nchini Morocco ni mkutano wa nne kufanyika barani Afrika.

Tags