Apr 22, 2016 16:28 UTC
  • Ban: Mkataba wa tabianchi ni kwa ajili ya vizazi vijavyo

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema jitihada za kupambana na mabadiliko ya tabianchi ni kwa ajili ya vizazi vijavyo, wakati ambapo kila siku rekodi za uchafuzi wa hali ya hewa zinavunjwa.

Ameyasema hayo leo Ijumaa katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa ambapo viongozi na wawakilishi wa nchi 171 za dunia wamekutana na wanatia saini mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi.

Ban Ki-moon baada ya kuwakaribisha viongozi na wawakilishi wa dunia katika hafla hiyo alimtambulisha na kumwachia jukwaa Gerturdue Clement, msichana mwenye umri wa miaka 16 kutoka Mwanza, Tanzania akisema jamii ya kimataifa inapaswa kusikiliza sauti za vijana. Gertrude aliwahimiza viongozi kuchukua hatua leo, wala si kesho.

Kwa upande wake Bwana Ban amesema siku hii ni ya kihistoria katika jitihada za kupambana na mabadiliko ya tabianchi kwa ajili ya vizazi vijavyo, wakati ambapo kila siku rekodi za uchafuzi wa hali ya hewa zinavunjwa.

Katibu Mkuu wa UN ameongeza kwamba ni lazima kusaidia nchi zinazoendelea kubadilisha chumi zao ili kuwa rafiki kwa mazingira.

Ban amekumbusha kuwa hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi si mzigo, bali inaweza kuleta faidia nyingi. Amesema hatua zinazochukuliwa sasa zinaweza kuchangia kutokomeza umaskini, kuzalisha ajira, kumaliza njaa, kuzuia mizozo na kuimarisha maisha ya wasichana na wanawake.

Tags