Nchi jirani na Kongo DR zatuhumiwa kukiuka makubaliano ya Addis Ababa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i19273-nchi_jirani_na_kongo_dr_zatuhumiwa_kukiuka_makubaliano_ya_addis_ababa
Kamati ya Utekelezaji Makubaliano ya Addis Ababa imezituhumu nchi jirani na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuwa zimekiuka makubaliano hayo kwa kuwapa hifadhi waasi wa zamani wa nchini humo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 11, 2016 15:50 UTC
  • Nchi jirani na Kongo DR zatuhumiwa kukiuka makubaliano ya Addis Ababa

Kamati ya Utekelezaji Makubaliano ya Addis Ababa imezituhumu nchi jirani na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuwa zimekiuka makubaliano hayo kwa kuwapa hifadhi waasi wa zamani wa nchini humo.

Denis Kalume, Mratibu wa Kamati ya Utekelazaji wa Makubaliano ya Addis Ababa amesema kuwa, baadhi ya nchi zilizosaini makubaliano hayo hazina nia ya kutekeleza ipasavyo vipengee vyake. Kalume amesisitiza kuwa viongozi wengi wa waasi wa zamani wa Harakati ya Machi 23 hivi sasa wanasakwa na mahakama moja ya Kongo.

Tarehe kumi mwezi Oktoba mwaka huu Denis Kalume aliteuliwa kuwa Mtaribu wa Kamati ya Utekelezaji wa Makubaliano ya Addis Ababa na kuchukua nafasi ya Francois Mwamba aliyejiuzulu.

Waasi wa zamani wa Machi 23 

Makubaliano ya Addis Ababa ambayo yalisainiwa Februari 24 mwaka 2013 mjini Addis Ababa yanaeleza kuwa, ni marufuku kuwapa hifadhi au kuwaunga mkono shakhsia wanaotuhumiwa kutenda jinai za kivita, jinai dhidi ya binadamu na mauaji ya halaiki.

Habari zinasema kuwa waasi wa zamani zaidi ya 1500 wa Harakati ya Machi 23 wamepewa hifadhi katika nchi za Rwanda na Uganda baada ya kupata pigo mwezi Novemba mwaka 2013 kutoka kwa jeshi la Kongo huko katika mji wa Goma mashariki mwa nchi hiyo.