Dec 15, 2016 04:30 UTC
  • Mafunzo ya Qur'ani katika Chuo Kikuu cha Kiislamu Gambia

Kituo cha Kuhifadhi Qur'ani Tukufu Gambia (GQMC) kinachofungamana na Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Intaneti cha Gambia kimeandaa masomo ya kuhifadhi Qur'ani kupitia intaneti kwa lengo la kutoa mafunzo kwa Waislamu kona zote za dunia.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, kituo hicho cha kuhifadhi Qur'ani Tukufu ambacho kinatoa mafunzo kwa Waislamu wote duniani bila kujali umri kinasimamiwa na maustadhi bingwa wa Qurani na kinatoa mafunzo yake yote ya kuhifadhi na qiraa ya Qur'ani kwa njia ya intaneti.

Kituo hiki kimeweka kategoria tatu kwa wanaoshiriki ambazo ni pamoja na kundi la wanaoanza, kundi la kati na kundi la waliofika daraja ya juu. Kila ambaye anajisajili kushiriki katika mafundisho hayo kwa njia ya intanetia anapata mwalimu maalumu wa kumfunza.

Kituo hiki cha kutoa mafunzo ya kuhifadhi Qur'ani pia kina mafundisho maalumu kwa wale  ambao hawafahamu lugha ya Kiarabu au ufahamu wao ni duni.

Kikao cha kusoma Qur'ani

Kituo cha Kuhifadhi Qur'ani Tukufu Gambia kilianzishwa mwaka 2011 kwa himaya ya Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Gambia  ambapo kina ratiba za mafundisho ya kuhifadhi Qur'ani kwa makundi na kwa mtu binafsi pamoja na mafundisho ya qiraa ya Qur'ani Tukufu na wanaohitimu hupata vyeti. Takribani asilimia 95 ya wakaazi wote milioni moja laki nane nchini Gambia ni Waislamu.

Tags