Dec 23, 2016 03:31 UTC
  • Balozi wa Russia Cairo: Qur'ani na Uislamu havina uhusiano wowote na ugaidi

Balozi wa Russia mjini Cairo, Misri amesema kuwa mafundisho ya Qur'ani tukufu hayana mfungamano wa aina yoyote ile ya ugaidi.

Sergei Kirpichenko amesisitiza kuwa, mafundisho ya Uislamu na Qur'ani yako mbali kabisa na ugaidi na kuongeza kuwa, Qur'ani imetaja suala la urehemevu kabla hata ya kuzungumzia uhuru na uadilifu. 

Balozi wa Russia mjini Cairo amesema kuwa, magaidi hawaelewi wala hawatambui rehma ya Qur'ani tukufu na kwamba, kwa hakika magaidi ni watu ambao wametoka kwenye dini. 

Balozi Sergei Kirpichenko amepongeza misimamo ya nchi mbalimbali zilizolaani mauaji ya balozi mwenzake wa Russia nchini Uturuki na kukisifu Kituo cha Kiislamu cha al Azhar kwa kutoa wito wa upendo, mahaba, amani na ushirikiano.

Balozi wa Russia Uturuki akiwa chini baada ya kupigwa risasi

Balozi wa Russia mjini Ankara, Andrey Karlov aliuawa juzi kwa kupigwa risasi kadhaa na mtu aliyetambuliwa kuwa afisa polisi wa Uturuki. Balozi Andrey Karlov aliuawa wakati alipokuwa akihutubia maonyesho ya sanaa ya picha mjini Ankara, Uturuki. 

 

Tags