Shakhsia wa kisiasa wa Tunisia kuelekea Syria kwenda kumwomba radhi Rais Assad
Ujumbe wa viongozi wa vyama vya siasa vya Tunisia unatazamiwa kuelekea nchini Syria kwa madhumuni ya kwenda kumwomba radhi Rais Bashar al-Assad wa nchi hiyo.
Duru za kuaminika za Tunisia zimeripoti kuwa hivi karibuni, Muhsin Marzuq, Katibu Mkuu wa Harakati ya Uhalali wa Kisiasa ya Tunisia anatazamiwa kuongoza ujumbe wa shakhsia kadhaa wa nchi hiyo katika safari ya kuelekea Syria kwenda kumwomba radhi Rais wa nchi hiyo Bashar al-Assad kwa niaba ya wananchi wa Tunisia kutokana na hitilafu za kisiasa zilizotokea kuhusiana na vita vya Syria.
Kwa mujibu wa duru hizo lengo la safari hiyo ni kwenda kusafisha taswira hasi katika fikra za wananchi wa Syria kuhusiana na Watunisia.
Tangu vilipoanza vita dhidi ya Syria mwaka 2011, Tunisia ilikuwa moja ya nchi zilizoshuhudia magaidi na wabeba silaha wenye uraia wa nchi hiyo wakifanya safari kuelekea Syria kwa lengo la kupigana vita dhidi ya serikali halali ya Rais Assad.
Kwa mujibu wa maafisa wa serikali ya Tunis, Watunisia wanaokadiriwa kufikia 3,000 wamejiunga na makundi ya kigaidi hususan Daesh na hivi sasa wanashiriki kwenye vita vinavyoendelea nchini Syria.
Mnamo mwezi Februari mwaka 2012, Tunisia ilivunja uhusiano wake wa kidiplomasia na Syria na kumfukuza balozi wa nchi hiyo aliyekuweko mjini Tunis.
Rais wa wakati huo wa Tunisia Mohamed Moncef Marzouki alitangaza kuwa njia pekee ya utatuzi wa mgogoro wa Syria ni kuondoka madarakani rais Bashar al-Assad, lakini baada ya chama cha Neda Tunis kuingia madarakani, Waziri wa Mambo ya Nje wa Tunisia Taieb Baccouche alisisitiza kuwa nchi hiyo imeamua kuanzisha tena shughuli zake za kidiplomasia mjini Damascus.
Katikati ya mwaka huu, baadhi ya duru za Wizara ya Mambo ya Nje ya Tunisia zilitangaza kuwa nchi hiyo imeanzisha tena uhusiano wa kidiplomasia na Syria; na Ibrahim al-Fawari ameteuliwa kuwa balozi mdogo wa Tunisia mjini Damascus…/