Ikhwanul Muslimin yakanusha kutaka maridhiano na serikali ya Misri
Katibu Mkuu wa harakati ya Ikhwanul Muslimin ya Misri amekanusha kutolewa ombi lolote na harakati hiyo la kutaka ufanyike usuluhishi baina yake na utawala wa sasa wa nchi hiyo.
Mahmoud Hussein ametangaza kuwa ripoti kwamba Ikhwanul Muslimin imemwomba Mkuu wa Kituo cha Mitaala cha Ibnu Khaldun Sa'aduddin Ibrahim achukue jukumu la kuipatanisha harakati hiyo na utawala ulioko madarakani nchini Misri hazina ukweli wowote.
Hussein ameongeza kuwa msimamo wa Ikhwanul Muslimin uko wazi kabisa; nao ni wa kutokubali uhalali wa kisheria wa serikali iliyopo na kusisitiza kurejeshwa madarakani Muhammad Morsi, rais aliyepinduliwa na jeshi. Aidha kutofikia maridhiano na watu ambao mikono yao imetapakaa damu za Wamisri na kutosamehe haki ya watu waliouliwa pamoja na kuhakikisha malengo ya mapinduzi ya wananchi ya Januari 25 mwaka 2011 yanafikiwa.
Siku chache zilizopita, baadhi ya vyombo vya habari vilidai kuwa hivi karibuni yalifanyika mazungumzo mjini Istanbul, Uturuki baina ya Sa'aduddin Ibrahim, Mkuu wa Kituo cha Mitaala cha Ibnu Khaldun na Katibu Mkuu wa Ikhwanul Muslimin Mahmoud Hussein yaliyohudhuriwa pia na Ayman Nour, kiongozi wa upinzani nchini Misri, na kwamba katika mazungumzo hayo Hussein alimwomba Ibrahim awe msuluhishi baina ya Ikhwanul Muslimin na utawala wa Misri.../