UN: Tutashirikiana na Gambia kuwashughulikia waliotenda jinai enzi za utawala wa Jammeh
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, uko tayari kushirikiana na serikali mpya ya Gambia katika masuala ya kimahakama na haki za binadamu.
Taarifa ya Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa, umoja huo uko tayari kushirikiana na serikali mpya ya Gambia endapo serikali hiyo itatoa ombi katika uwanja huo ili kuhakikisha kwamba, wale wote waliotenda jinai na kukiuka haki za binadamu katika kipindi cha uongozi wa Yahya Jammeh, rais wa zamani wa nchi hiyo wanapandishwa kizimbani.
Hayo yameelezwa na Jeffrey Feltman, Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Kisiasa katika safari yake nchini Gambia ambapo amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wa nchi hiyo.
Katika mazungumzo yake na Rais Adama Barrow wa Gambia, Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza udharura wa kuweko maridhiano ya kitaifa baina ya makundi ya kisiasa ya nchi hiyo na vilevile kutekelezwa uadilifu kuhusiana na watenda jinai.
Siku chache zilizopita, shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch lilitoa ripoti iliyoeleza kwamba, serikali ya Jammeh ilikuwa ikitumia vitisho na utesaji dhidi ya viongozi wa vyama vya upinzani na wakosoaji sambamba na kuwanyima haki zao za msingi.
Yahya Jammeh aliyeitawala Gambia kwa kipindi cha miaka 22 aliondoka madarakani kutokana na mashinikizo ya walimwengu, baada ya hatua yake ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais uliofanyika Disemba mwaka jana, ambayo awali aliyakubali.