Muungano wa upinzani Kenya wamtangaza Raila Odinga kuwa mgombea wake wa urais
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i28332-muungano_wa_upinzani_kenya_wamtangaza_raila_odinga_kuwa_mgombea_wake_wa_urais
Muungano mkuu wa upinzani nchini Kenya NASA, hatimaye leo umemtangaza mgombea wake wa urais aliyekuwa akisubiriwa kwa muda mrefu. Muungano huo umemtangaza kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kuwa mgombea wake wa urais katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Agosti 8 mwaka huu.
(last modified 2026-04-23T06:05:17+00:00 )
Apr 27, 2017 11:33 UTC
  • Muungano wa upinzani Kenya wamtangaza Raila Odinga kuwa mgombea wake wa urais

Muungano mkuu wa upinzani nchini Kenya NASA, hatimaye leo umemtangaza mgombea wake wa urais aliyekuwa akisubiriwa kwa muda mrefu. Muungano huo umemtangaza kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kuwa mgombea wake wa urais katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Agosti 8 mwaka huu.

Hii itakuwa ni mara ya nne kwa Odinga, mwenye umri wa miaka 72 kuwania urais wa Kenya.

Katika hafla iliyofanyika kwenye uwanja wa kihistoria wa Bustani ya Uhuru Park jijini Nairobi na kuhudhuriwa na maelfu ya wafuasi wa muungano huo, Raila alitajwa kuwa mgombea urais wa NASA na Kalonzo Musyoka mgombea wake mwenza ili kuchuana na Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi mkuu wa Agosti 8.

Katika hotuba aliyotoa baada ya kuteuliwa, Raila Odinga ameahidi kushusha bei za vyakula na kupambana na ufisadi. Aidha ameahidi kuifanyia mabadiliko sekta ya umma na kuwepo serikali za mitaa zenye nguvu zaidi.

Hata hivyo kutokana na muundo wa mgao wa madaraka uliopangwa na muungano wa NASA, Raila hatokuwa na madaraka mutlaki endapo atachaguliwa kuwa rais mpya wa Kenya katika uchaguzi mkuu wa tarehe 8 Agosti.

Vinara wa NASA. Kutoka kushoto: Moses Wetangula, Raila Odinga, Kalonzo Musyoka na Musalia Mudavadi

Katika muundo huo, kiongozi wa chama cha Amani Musalia Mudavadi atakuwa Waziri Kiongozi anayehusika na Uratibu wa Serikali. Naye kiongozi wa chama cha Ford Kenya Moses Wetangula atakuwa Naibu Waziri Kiongozi anayehusika na uratibu wa sekta ya uchumi. Kiongozi wa Chama cha Mashinani Isaac Ruto, atakuwa Naibu mwengine wa Waziri Kiongozi, atakayehusika na utawala na uratibu wa sekta ya huduma za jamii.

Muundo huo wa makubaliano yaliyofikiwa baina ya vyama tanzu vinavyounda muungano wa upinzani wa NASA unaonyesha kuwa rais atagawana madaraka na washirika wake wakuu ikiwemo katika suala la uteuzi wa baraza la mawaziri kupitia mashauriano na makubaliano.../