Kofi Annan Foundation: Yumkini Kenya ikatumbukia katika ghasia za Uchaguzi Mkuu 2027
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i139908-kofi_annan_foundation_yumkini_kenya_ikatumbukia_katika_ghasia_za_uchaguzi_mkuu_2027
Ripoti mpya iliyotolewa na taasisi ya Kofi Annan Foundation imeonya kuwa nchi ya Kenya iko katika hatari kubwa ya kushuhudia vurugu zinazohusiana na uchaguzi mkuu wa 2027 iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.
(last modified 2026-07-16T02:54:36+00:00 )
Jul 16, 2026 02:48 UTC
  • Kofi Annan Foundation: Kenya iko kwenye hatari ya ghasia za uchaguzi 2027.
    Kofi Annan Foundation: Kenya iko kwenye hatari ya ghasia za uchaguzi 2027.

Ripoti mpya iliyotolewa na taasisi ya Kofi Annan Foundation imeonya kuwa nchi ya Kenya iko katika hatari kubwa ya kushuhudia vurugu zinazohusiana na uchaguzi mkuu wa 2027 iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.

Ripoti hiyo inakadiria kuwa kuna uwezekano wa asilimia 81.6 wa kutokea ghasia za uchaguzi nchini Kenya.

Ingawa Kofi Annan Foundation inasema Kenya imepiga hatua kubwa tangu ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007/2008, lakini inaonya kuwa mizizi ya migogoro hiyo bado haijang’olewa.

Imesema kuna mkusanyiko wa sababu mbalimbali zinazochochea machafuko hayo kama vile ukosefu wa uvumilivu wa kisiasa, siasa za ukabila, ugumu wa maisha, ukosefu wa ajira kwa vijana, kupungua imani kwa taasisi za umma na kuongezeka kwa makundi ya wahuni wanaotumiwa na wanasiasa.

Ripoti hiyo imesema, Kenya ina taasisi imara zaidi kuliko mataifa mengi yaliyo katika hatari kubwa ya migogoro ya uchaguzi lakini inaonya kuwa taasisi hizo zinaendelea kupoteza uaminifu wa wananchi kutokana na migawanyiko ya kisiasa, malalamishi ambayo hayajatatuliwa na wasiwasi kuhusu kutopendelea upande wowote kwa baadhi ya taasisi za serikali.

Ripoti ya Kofi Annan Foundation inaeleza kuwa tangu uchaguzi wa 2022 nchini Kenya, mazingira ya kisiasa yamekuwa yakitawaliwa na ugumu wa maisha, maandamano dhidi ya ushuru, hasira kuhusu ufisadi na mwenendo wa polisi pamoja na maandamano ya vijana yaliyotokea nje ya miundo ya kawaida ya vyama vya kisiasa.

Wataalamu wa taasisi hiyo wanashauri polisi wapewe mafunzo zaidi kuhusu namna ya kudhibiti umati bila kutumia nguvu kupita kiasi na kuhakikisha wanabaki huru kisiasa.

Vilevile, wanaitaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya (IEBC) kuchapisha mapema ratiba ya shughuli zake, utaratibu wa usajili wa wapigakura, ununuzi wa teknolojia ya uchaguzi na namna matokeo yatakavyosimamiwa ili kuondoa hofu na uvumi.