Serikali ya Kenya yaja na mpango wa kuimarisha utalii 'Halal'
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i28466-serikali_ya_kenya_yaja_na_mpango_wa_kuimarisha_utalii_'halal'
Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya imeazimia kuimarisha utalii 'Halal' ambao unalenga kuwavutia watalii Waislamu kwa kutoa huduma ambazo zinazingatia mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 30, 2017 11:44 UTC
  • Serikali ya Kenya yaja na mpango wa kuimarisha utalii 'Halal'

Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya imeazimia kuimarisha utalii 'Halal' ambao unalenga kuwavutia watalii Waislamu kwa kutoa huduma ambazo zinazingatia mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu.

Waziri wa Utalii Kenya Najib Balala amenukuliwa na Shirika la Habari la Kimataifa la Quráni Tukufu IQNA akisema kuwa, serikali ya Nairobi imechukua hatua zote zinazohitajika ili kustawisha utalii Halal na tayari hatua zimeshachukuliwa za kubuni sheria maalumu kwa ajili ya utalii huo.

Majengo ya kihistoria ni miongoni mwa vivutio vikubwa vya watalii nchini Kenya

 

"Tokea serikali hii iingie madarakani, imechukua hatua mbalimbali za kubuni sheria za utalii Halal na halmasharui husika zimeshapewa amri ya kutekeleza jambo hilo. Zamani tulikuwa tunapoteza watalii wengi, hasa kutoka nchi za Kiarabu, kwa sababu ya kukosa huduma halali lakini sasa tunaanzisha hoteli zenye kutoa huduma hizo. Aidha wafanyakazi wa hoteli hizo wanapewa mafunzo maalumu yanayohusu huduma Halal za kitalii," amesema waziri Balala.

Halikadhalika waziri huyo wa utalii Kenya amesema kuwa, hoteli zitakazokuwa zinatoa huduma Halal zitakuwa kwa mfano zina sehemu tafauti za kuogolea za wanaume na wanawake na mfumo mzima wa upishi utazingatia kikamilifu chakula halali. Aidha hoteli hizo zimepangiwa kuwa na sehemu maalumu za kuswalia na hakutakuwa na ruhusa wa kuingizwa pombe au kufanyika tabia zisizo za Kiislamu katika hoteli hizo ili kuwavutia watalii Waislamu kutoka kote duniani. Aidha watalii wanaofadhilisha kutekeleza ibada za Mwezi Mtukufu wa Ramadhani nchini Kenya watapata huduma maalumu za mwezi huo katika hoteli zenye huduma za Halal.

 

Balala amesisitiza kuwa serikali ya sasa ya Kenya inalipa umuhimu mkubwa suala la hisia za Waislamu kuliko wakati mwingine wowote.

Kwa upande wake, Mohammad Hersi, Mkuu wa Jumuiya ya Utalii ya Eneo la Pwani huko Kenya amesema kuwa, kutokana na kuweko turathi ya Kiislamu katika eneo la Pwani nchini Kenya, eneo hilo linaweza kuwa kivutio kikubwa kwa watalii Waislamu wanaotaka huduma Halal.

Amongeza kuwa: "Sekta ya utalii Halal inastawi kwa kasi zaidi duniani huku takwimu zikionyesha kuwa Waislamu wanaokwenda safari za kitalii wanazidi kuongezeka. Kwa mfano mwaka 2015, Kenya ilipokea watalii 40,875 kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu ikiwa ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na mwaka wa kabla yake ambapo Kenya ilipata watali 24,828 kutoka nchi hiyo."