Wakenya wamshangaa Raila Odinga kuuombea utawala wa Kizayuni wa Israel
Hatua ya mgombea wa urais wa Muungano wa National Super Alliance (NASA) Raila Odinga ya kuiombea Israeli, wakati alipofanya safari huko Quds hapo jana, imewashangaza Wakenya wengi katika mitandao ya kijamii.
Akiwa huko Quds ambao ni mji mkuu wa Palestina, Odinga alizuru ukuta unaodaiwa na Wazayuni kuwa ni mabaki ya Hekalu bandia la Nabii Sulemani (as) ambapo pia alionekana akiweka kikaratasi katika ufa wa ukuta huo.
Hii ni kwa kuwa mbali na madai hayo ya Wazayuni kukosolewa mara kadhaa na asasi za kimataifa likiwemo Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) na kuthibitisha kuwa eneo hilo linahusiana na Waislamu pekee, Israel pia inatambuliwa duniani kuwa ni utawala wa kwanza kufanya ukandamizaji na kila aina ya jinai dhidi ya binaadamu. Baadhi ya Wakenya wamelaani kitendo hicho cha mwanasiasa huyo na kuitaja hatua yake kuwa ni kuunga mkono ukandamizaji unaofanywa kila uchao na Israel dhidi ya Wapalestina.
Kulingana na picha alizozituma katika akaunti yake ya Facebook, Odinga alionekana akiomba huku akiwa amevalia kijikofia cheupe kichwani, kama wanavyoabudu Mayahudi. Kwa mujibu wa imani potofu ya Wazayuni, maombi yanayoandikwa katika kijikaratasi na kuwekwa kwenye ufa wa ukuta huo wa Western Wall yanamfikia Mungu moja kwa moja mbinguni.