Mlipuko wa kipindupindu wauawa watu 7 nchini Kenya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i29284-mlipuko_wa_kipindupindu_wauawa_watu_7_nchini_kenya
Kwa akali watu wanne wameripotiwa kufariki dunia kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu nchini Kenya, huku mji mkuu Nairobi ukiathiriwa zaidi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 19, 2017 03:27 UTC
  • Mlipuko wa kipindupindu wauawa watu 7 nchini Kenya

Kwa akali watu wanne wameripotiwa kufariki dunia kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu nchini Kenya, huku mji mkuu Nairobi ukiathiriwa zaidi.

Bernard Muia, Waziri wa Afya wa serikali ya kaunti ya Nairobi amesema watu watatu wanadaiwa kupoteza maisha kutokana na ugonjwa huo katika mtaa wa Komarock, viungani mwa mji huo.

Kadhalika Mkurugenzi wa Afya nchini Kenya, Quido Ahindukha amesema mtu mmoja ameaga dunia kutokana na mlipuko wa ugonjwa huo katika kaunti ya Vihiga, magharibi mwa nchi, huku wagonjwa wawili katika Hospitali Kuu ya Kaimosi eneo hilo wakitibiwa na kuruhusiwa kuondoka hospitalini.

Habari ambazo hazijathibitishwa zinasema watu wengine watatu wameaga dunia kutokana na ugonjwa huo katika mtaa wa Kayole jijini Nairobi.

Ukosefu wa maji safi ya kunywa unachangia kuenea kwa kipindupindu

Wizara ya Afya nchini Kenya imetoa tahadhari kuhusu kuenea kwa kasi kwa ugonjwa huo, hususan katika mji mkuu Nairobi. 

Mwezi uliopita, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilisema kuwa, kesi zaidi 21,000 za kipindupindu zimeripotiwa katika nchi jirani ya Somalia na kwamba watu 533 wamefariki dunia kutokana na ugonjwa huo huko Somalia tangu mwanzo wa mwaka huu.

Machi mwaka huu, Ripoti ya UNICEF iliyotolewa kwa mnasaba wa Siku ya Maji Duniani ilionyesha kuwa, watoto zaidi ya 800 wanapoteza maisha kila siku katika sehemu tofauti za dunia, kutokana na ugonjwa wa kuharisha, unaosababishwa na mazingira machafu na ukosefu wa maji safi ya kunywa.