WHO: Matumizi ya tumbaku yanaua watu milioni 7 kila mwaka duniani
Shirika la Afya Duniani WHO limesema watu zaidi ya milioni saba wanafariki dunia kila mwaka kutokana na matumizi ya tumbaku kote duniani.
Katika taarifa aliyotoa kwa mnasaba wa Siku ya Dunia Bila ya Tumbaku inayoadhimishwa leo Jumatano, sawa na tarehe 31 Mei kila mwaka, Margaret Chan, Mkuu wa WHO amesema matumizi ya tumbaku mbali na kusababisha maafa, yanaongeza viwango vya umasikini, kupunguza ukuaji wa uchumi, kuvunja nyumba, mbali na kuchafua mazingira.
Takwimu za sasa zinaonesha ongezeko kubwa, ikizingatiwa kuwa, takwimu za mwaka jana zilionyesha kuwa watu milioni sita wanapoteza maisha kila mwaka kwa matumizi ya bidhaa za tumbaku, mbali na wengine laki sita wanaofariki kutokana na athari ya moshi wa wavutaji sigara.
Mkuu wa Shirika la Afya Duniani amesema ongezeko hilo linatia wasiwasi licha ya kampeni zinazofanywa kote duniani. Amefafanua kuwa, takwimu hizo zinazidi kupanda kila mwaka, kwani matumizi ya tumbaku yalisababisha vifo vya watu milioni 4 kila mwaka muongo mmoja uliopita na kwamba yumkini watu bilioni moja watakuwa wemepoteza maisha kutokana na matumizi hayo kufikia mwishoni mwa karne hii.
WHO inakadiria kuwa, takriban dola trilioni 1.4 za Marekani zinatumika kila mwaka kote duniani, kwa ajili ya matibabu ya magonjwa yanayosababishwa na matumizi ya sigara na bidhaa nyingine za tumbaku.