WHO: Uvutaji sigara unahatarisha afya ya watu bilioni 1.2 duniani kote
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza takwimu za kutisha na za kusikitisha kuhusu hatari ya uvutaji sigara, kwa mnasaba wa madhimisho ya kila mwaka ya Siku ya Kupiga Vita Tumbaku Duniani, ambayo huadhimishwa Mei 31.
Mwaka huu, shirika hilo limetangaza kwenye tovuti yake kwamba watoto milioni 40 kote duniani wanatumia tumbaku za aina mbalimbali, wakiwemo vijana milioni 15 wenye kati ya umri wa miaka 13 na 15 wanaotumia sigara za kielektroniki.
Inakadiriwa kuwa kuna takriban watumiaji bilioni 1.2 wa tumbaku duniani, 80% kati yao wakiishi katika nchi zenye kipato cha chini au cha kati.
Mbali na madhara ya kiafya ya tumbaku, jumla ya gharama za kiuchumi za kutibu madhara ya kiafya na kijamii ya uvutaji sigara inakadiriwa kuwa takriban dola za Marekani trilioni 1.4 kila mwaka, au 1.8% ya Pato la Taifa la kimataifa, huku nchi zinazoendelea zikibeba takriban 40% ya gharama hizi.
Mwaka huu, Shirika la Afya Duniani (WHO) limeibua kauli mbiu "Kufichua Vivutio vya Uongo - Kupambana na Uraibu wa Tumbaku na Nikotini" ili kuongeza uelewa wa hatari za tumbaku na kupunguza kasi ya kuenea kwake miongoni mwa makundi yote, hasa vijana wenye umri mdogo na kulinda kizazi kipya kutokana na uraibu wa bidhaa za tumbaku na nikotini, ambao wamedanganywa kwa kampeni kubwa za matangazo zinazofanywa na makampuni ya uzalishaji na utengenezaji wa tumbaku na sigara kote duniani.
Shirika la Afya Duniani limeonya kuhusu mbinu hatari inayotumiwa na makampuni ya tumbaku na nikotini, ambayo hutegemea mbinu ya uhandisi bidhaa zao ili kuzifanya zivutie zaidi na rahisi kutumia, na iwe vigumu kwa wavutaji sigara kuacha tabia hiyo, hasa miongoni mwa vijana na barobaro. Mwishowe, makampuni hayo hupata faida kubwa kwa gharama ya kizazi kipya cha vijana ambao huwa waraibu wa tumbaku na aina mbalimbali za bidhaa zake zote.
Shirika la Afya Duniani limetoa wito kwa serikali kuwalinda raia wao kwa kupiga marufuku bidhaa za tumbaku zilizotiwa ladha au kiungo fulani, kupiga marufuku matangazo ya tumbaku na bidhaa zake, kufanya maeneo ya umma yaliyofungwa yasiwe na uvutaji tumbaku na sigara za kielektroniki, na kuimarisha utekelezaji wa sheria.
Shirika hilo linasema tumbaku husababisha vifo vya zaidi ya watu milioni 7 duniani kote kila mwaka, ikiwa ni pamoja na watu milioni 1.6 wasiovuta sigara ambao huvuta moshi wa mvuta sigara, au ule unaojulikana kama uvutaji sigara hasi.
Baadhi ya tafiti zinaonyesha kuwa moshi wa sigara una zaidi ya kemikali 7,000, ikiwa ni pamoja na kwa uchache mada 69 zinazosababisha kansa. Kwa hivyo, moshi huo hauwaathiri tu wavutaji sigara moja kwa moja, lakini pia unahatarisha uhai wa wale walio karibu nao kupitia uvutaji sigara hasi.
Uvutaji sigara unasalia kuwa mojawapo ya sababu kuu za vifo duniani kote, kwani una uhusiano wa karibu na magonjwa ya moyo na mishipa na magonjwa ya kupumua, pamoja na kuwa chanzo kikuu cha zaidi ya aina 20 za saratani.