Mkurugenzi Mkuu wa WHO: Vifo vinavyoshukiwa kuwa vya Ebola vyafika 220
-
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dr Tedros Adhanom
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ameeleza kuwa vifo 220 vinashukiwa kusababishwa na mlipuko wa sasa wa homa hatari ya Ebola.
"Tumezidisha operesheni kwa haraka, lakini kwa sasa janga hilo linatuzidi," Tedros Adhanom Ghebreyesus ameeleza haya jana Jumatatu, na kuongeza kuwa: Nchi zinazopakana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) zinapaswa kuchukua hatua mara moja.
Mapema siku ya Jumatatu, Uganda iliripoti watu wawili zaidi kuambukizwa Ebola, na hivyo kupelekea jumla ya wagonjwa walioambukizwa kufikia saba.
Tedros Gebreyesus Adhanom Jumapili aliandika katika akaunti yake ya mtandao wa kijami kwamba juhudi za ufuatiliaji wa maambukizi nchini Kongo zimeongezeka akisema zaidi ya kesi 900 zinazoshukiwa zimetambuliwa hadi sasa.
Ebola ni ugonjwa unaosababishwa na virusi ambao huenea kwa kugusana moja kwa moja na maji yanayotoka katika mwili wa mgonjwa. Ugonjwa huo husababisha kuvuja damu nyingi na mwili kudhoofisha na hatimaye mgonjwa kuaga dunia.
Kitovu cha mlipuko wa sasa wa Ebola kimeripotiwa katika jimbo la Ituri kaskazini-mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mlipuko huo umeenea pia katika majimbo ya jirani, hadi umbali wa kilomita 200 na pia nje ya mipaka ya nchi hiyo, hadi Uganda.