Makubaliano kuhusu njia za kukabiliana na wahajiri haramu wa Afrika
Katika kuendelea kukabiliana na wahajiri haramu, wawakilishi wa nchi 10 za Kiafrika, Ulaya na asasi nne za kieneo wamekubaliana kuhusu njia za kukabiliana na wahajiri hao haramu kupitia Bahari ya Mediterania na kuimarisha ushirikiano ili kuwazuia wahajiri hao.
Washiriki wa mkutano wa kujadili tatizo la wahajiri haramu uliofanyika nchini Tunisia sambamba na kukiri kwamba, hakuna nchi ambayo inaweza kupambana peke yake la tatizo la wahajiri haramu wamesisitiza juu ya udharura wa kuweko ubadilishanaji taarifa kuhusiana na mitandao ya magendo ya binadamu na wahajiri na nchi zote kufanya uchunguzi kuhusiana na chanzo na sababu za kuweko uhajiri haramu.
Katika miaka ya hivi karibuni kiwango cha wahajiri haramu wanaotoka katika nchi mbalimbali za Kiafrika kwa lengo la kuelekea barani Ulaya ili kutafuta maisha kimeshuhudiwa kikiongezeka mno. Matatizo ya kisiasa, vita, mapigano ya ndani, na harakati za makundi ya kigaidi ni mambo ambayo yamesababisha kuongezeka ukosefu wa amani na usalama katika akthari ya nchi za Kiafrika.
Katika upande mwingine, matatizo ya kiuchumi, umasikini, ukosefu wa ajira, kutokuweko usalama wa chakula kutokana na mabadiliko ya tabianchi sambamba na vita, ni mambo ambayo kwa hakika yameyafanya maisha ya baadhi ya nchi za Kiafrika kuwa magumu mno.
Matatizo hayo yakiwa ni ya upande mmoja, ambapo katika upande wa pili ni kuwa, mazingira yanayotawala hivi sasa nchini Libya na kutokuweko serikalii kuu yenye nguvu na inayoweza kudhibiti mipaka yake, ni suala ambalo limepelekea raia wengi wa Kiafrika hususan vijana kuichagua nchi hiyo kama njia yao ya mkato ya kuelekea barani Ulaya kwa ajili ya kutafuta maisha bora.
Wahajiri hao haramu hukumbana na matatizo mengi njiani na wengine kupoteza maisha. Wimbi hili la wahajiri haramu, limepelekea pia kuongezeka magenge ya magendo ya binadamu katika eneo.
Ripoti zinaonyesha kuwa, wengi wa wahajiri hao hufa maji wakati wakiwa katika jitihada za kuvuka Bahari ya Mediterania ili kuelekea barani Ulaya au huangukia mikononi mwa magenge yanayojihusisha na magendo ya binadamu na hivyo kuwa wahanga wa makundi hayo.
Katika upande mwingine, wahajiri haramu kwa miaka kadhaa sasa wamekuwa ni changamoto kubwa kwa Umoja wa Ulaya na kuufanya umoja huo ulazimike kutekeleza sera nje ya eneo kwa ajili ya kudhibiti wimbi la wahajiri hao. Kuwapatia makazi wahajiri hao katika nchi ambayo ni kituo cha kwanza cha wahajiri hao kabla ya kuwasili Ulaya au kuwatafutia nchi nyingine ya tatu kwa ajili ya makazi ni sehemu ya siasa za nchi wanachama wa umoja huo.
John Dalhuisen, Mkurugenzi Kitengo cha Ulaya cha Shirika la Msamaha la Amnesty International sambamba na kukosoa utendaji wa Umoja wa Ulaya amesema kuwa: Badala ya nchi za Ulaya kutafuta njia za kuokoa roho na maisha ya wahajiri na kuwaunga mkono, viongozi wa nchi hizo bila haya wala aibu wamekuwa wakijadili namna ya kukwamisha safari za wahajiri kuanzia katika nchi ambayo ni kituo chao cha kwanza.
Utafiti unaonyesha kuwa, mipango ya kukabiliana na wahajiri haramu hadi sasa haijawa na mafanikio; hasa kutokana na kuwa, matatizo ya kimsingi yanayozikabili nchi za Kiafrika chimbuko lake ni athari za siasa za miaka mingi za madola ya kikoloni ya Magharibi na uingiliaji wao katika masuala ya ndani ya nchi hizo.
Mintarafu hiyo, inaonekana kuwa, tatizo la wahajiri haramu wa Kiafrika litapatiwa ufumbuzi pale tu madola ya Magharibi yatakapotazama upya siasa zao mkabala na nchi za Kiafrika na kupunguza uingiliaji wao katika masuala ya ndani ya nchi hizo.
Kurejea usalama na uthabiti katika nchi zinazokabiliwa na migogoro barani Afrika hususan Libya, inaweza kuwa hatua ya kwanza kubwa ya kuelekea katika kulipatia ufumbuzi tatizo la wahajiri haramu.