Rais Buhari arejea Nigeria baada ya kuwa nje kwa miezi mitatu
Hatimaye Rais Muhamadu Buhari wa Nigeria amerejea nyumbani katika mji mkuu Abuja, baada ya kuwa nje ya nchi kwa miezi mitatu akipata matibabu katika mji mkuu wa Uingereza London.
Rais wa Nigeria amekuwa akiugua kwa muda mrefu sasa ingawa haijawekwa wazi maradhi hasa anayougua kiongozi huyo.
Furaha nderemo na vifijo vilitanda katika uwanja wa ndege wa Abuja wakati wafuasi wake walipokuja kumlaki kiongozi huyo.
Hadi sasa serikali na familia ya Buhari haijaweka wazi kuhusu ugonjwa unaomsumbua rais huyo wa Nigeria mwenye umri wa miaka 74. Rais Buhari anatarajiwa kuhutubia taifa kesho asubuhi. Kumekuwa na maandamano ya kumtaka Buhari arudi nyumbani au ajiuzulu.
Hivi karibuni Wanigeria walifanya maandamano makubwa yaliyoitishwa na jumuiya za kiraia wakipinga kitendo cha rais wa nchi hiyo kuendelea kuishi nje ya nchi kwa kipindi cha miezi mitatu.
Rais Buhari anarejea Nigeria huku nchi yake ikikabiliwa na changamoto mbalimbali likiwemo suala la ukosefu wa usalama kutokana na kushadidi mashambulio ya wanamgambo wa kundi la kigaidi la Boko Haram.
Serikali ya Rais Muhamadu Buhari inakosolewa vikali kwa kushindwa kukabiliana na kundi la Boko Haram. Hata kikosi cha pamoja cha nchi za eneo kilichoundwa kwa shabaha ya kukabiliana na wanamgambo hao wa Boko Haram kinaonekana kushindwa kufikia malengo yake.