Panya wavamia ofisi ya rais Nigeria, kikao cha baraza la mawaziri chaahirishwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i33530-panya_wavamia_ofisi_ya_rais_nigeria_kikao_cha_baraza_la_mawaziri_chaahirishwa
Kikao cha kwanza cha baraza la mawaziri Nigeria ambacho kilikuwa kifanyike leo baada ya kurejea nyumbani Rais Muhammadu Buhari kutoka likizo ya miezi mitatu ya kitiba Uingereza kimeahirishwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 23, 2017 09:28 UTC
  • Panya wavamia ofisi ya rais Nigeria, kikao cha baraza la mawaziri chaahirishwa

Kikao cha kwanza cha baraza la mawaziri Nigeria ambacho kilikuwa kifanyike leo baada ya kurejea nyumbani Rais Muhammadu Buhari kutoka likizo ya miezi mitatu ya kitiba Uingereza kimeahirishwa.

Msemaji wa Buhari, Femi Adesina ametoa habari za kuahirishwa kikao hicho cha baraza la mawaziri pasina kutoa maelezo zaidi.

Buhari alirejea Nigeria Jumamosi baada ya kusafiri Mei 7 kuelekea Uingereza kwa ajili ya matibabu ingawa ugonjwa wake hadi sasa haujatangazwa rasmi. Buhari aliwaandikia barua wabunge Jumatatu akiwajulisha kuwa amerejea na ameanza kazi zake.

Hayo yanajiri wakati ambao jana ilitangazwa kuwa Buhari atafanyia kazi nyumbani kwake kwa wiki tatu baada ya kurudi nchini humo kufuatia ziara ya matibabu nchini Uingereza. Hii ni baada ya panya kuvamia na kuharibu afisi yake.

Rais Buhari akirejea nyumbani Nigeria baada ya matibabu ya miezi mitatu London

Msemaji wa rais alisema kwamba ofisi ya Buhari inakarabatiwa baada ya panya kuharibu fanicha na kiyoyozi ndani ya afisi hiyo.

Aliongeza kuwa huku ikiwa Bwana Buhari hawezi kufanya kazi katika afisi yake kutokana na hali ya afisi yake kwa sasa, hatua yake ya kufanyia kazi nyumbani haitaathiri kivyovyote vile utendakazi wake.

Wakati akipata matibabi Uingereza, Buhari alikabidhi hatamu za uongozi kwa makamu wake, Yemi Osinbajo. Pamoja na kuwa kikao cha baraza la mawaziri kimeakhirishwa, Buhari leo anatazamiwa kupokea ripopti ya ufisadi wa maafisa wawili wa ngazi za juu serikalini.